Habari Mseto

Odibet yatatua tatizo la maji Makueni

February 29th, 2024 2 min read

NA JOHN ASHIHUNDU

TATIZO la ukosefu wa maji katika shule ya Kako School for Special Needs iliyoko Kaunti ya Makueni, limesuluhishwa kufuatia mradi mkubwa wa Odi Mtaani Foundation.

Kampuni ya Odibet ikishirikiana wa Bodi ya Kitaifa ya Kusimamia Leseni za Kamari (BCLB) kupitia kwa mpango wao wa Majukumu ya Shirika la Kijamii (CSR) imesema mradi huu muhimu kupitia kwa kitengo chake cha Odi Mtaani Foundation utasaidia shule hii pamoja na wakazi wa eneo hili kwa jumla.

Meneja Mkuu wa Odi Mtaani Dedan Mungai pamoja na mwenyekiti wa BCLB Jane Mwikali Makau wageni hao walisema mradi huo katika shule hiyo ya Mahitaji Maalum vile vile umeanzishwa kwa minajili ya kufanikisha jamii inayoishi katika eneo hilo.

Meneja Mkuu wa Odi Mtaani Dedan Mungai (kulia) pamoja na mwenyekiti wa BCLB Jane Mwikali Makau wakiwa katika Kaunti ya Makueni. PICHA | HISANI

Mkazi wa eneo hilo, Shadrack Nduto Mwendo alitoa asante kwa niaba ya wakazi, huku akieleza shukrani za dhati kwa uzinduzi wa mradi huo muhimu.

“Mradi huu utachangia katika ukuzaji elimu kwa kiasi kikubwa katika shule ya Kako pamoja na wananchi wa eneo hili ambao wamelalamika kukosa huduma hii muhimu. Tumekuwa tukitumia pesa nyingi kunuanua maji kwa bei ghali kwa ajili ya mautumizi yetu ya kila siku,” aliongeza Bw Mwendo.

Bw Mungai naye alieleza shukrani zake kwa kusema, “Tunawashukuru kwa makaribisho makubwa ambayo mmetupa. Tuna furaha ya kutoa msaada huu, lakini huu sio mwisho. Tutaendelea kuunga mkono jamii zote.”

Meneja Mkuu wa Odi Mtaani Dedan Mungai akihutubu. PICHA | HISANI

Alitangaza mwanzo kuchimba kisima cha maji kwa niaba ya timu ya Jiolojia uualioanza rasmi Jumatatu. Mbali na mradi huo, Odi Mtaani ilipeana taulo za kuchangia usafi pamoja na vyakula, huku akisisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo kuinua maendeleo ya jamii.

Bi Makau alisifu Odi Mtaani kwa ishara hiyo nzuri ambayo alisema inapaswa kukumbatiwa.

“Ningependa kushukuru Odi Mtaani Foundation kwa kuzindua mradi huu wa kuchimba kisima kusaidia shule hii pamoja na wakazi wa eneo hili kwa jumla,” akasema Bi Makau.

Alieleza zaidi na kushauri shule hiyo kuunda kamati kuu ya kuhakikisha mradi huo muhimu utakoacha alama isiyofutika unafanikiwa kwa faida ya shule na jamii inayoishi katika eneo hilo.

Hafla hiyo ilimalizika kwa upanzi wa miti, ikiongozwa na mgeni wa heshima pamoja na watu wengine mashuhuri walioalikwa kushuhudia kuzinduliwa kwa mradi huo wa kuinua jamii.

Odi Mtaani umeanzisha mradi ambao uthabiti wake utakuwa mfano mkubwa kwa kampuni nyingine zilizo na uwezo wa kusaidia jamii.

Wahudumu wa bodaboda wakifurahia jaketi spesheli za Odi Mtaani. PICHA | HISANI