ODM kumenyana na UDA Bondeni

ODM kumenyana na UDA Bondeni

Na VITALIS KIMUTAI

CHAMA cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, kimepiga hatua na chatarajiwa kutoana jasho na United Democratic Alliance (UDA), cha Naibu Rais William Ruto eneo la Rift Valley kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Vyama hivyo viwili, pamoja na kile cha Kanu cha seneta wa Baringo, Gideon Moi, ndivyo vyama vikubwa vya kisiasa vinavyomenyana kupata kura nyingi katika eneo hilo, ngome ya Dkt Ruto.

Dkt Ruto, Bw Odinga na Bw Moi wametangaza azma ya kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapoondoka mamlakani muhula wake wa pili utakapokamilika baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Vyama vya Jubilee, Amani National Congress cha Musalia Mudavadi, Wiper cha Bw Kalonzo Musyoka na Democratic Party ambacho kimemteua Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kupeperusha bendera yake, havijakuwa vikifanya kampeni katika eneo hilo.

Vyama vingine vidogo vyenye mizizi eneo hilo kama Chama Cha Mashinani (CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Isaac Ruto na Kenya United Party (KUP) cha Gavana wa Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo, pia havijapata ufuasi kama wa UDA, ODM na Kanu.

Dkt Ruto, Bw Odinga na Bw Moi wamekuwa wakitembelea eneo hilo wakijipigia debe kabla ya uchaguzi mkuu ujao kwa kukutana na na wajumbe, kuhudhuria ibada makanisani, kuongoza harambee na kufanya mikutano ya kisiasa.

Washirika wa Dkt Ruto wanasema kwamba uchaguzi mkuu unapokaribia, wanasiasa wengi watajiunga na UDA kabla ya mchujo wa vyama vya kisiasa.

“Tunapokaribia uchaguzi mkuu ujao na kwa kuzingatia miungano ya kisiasa inavyoendelea kuchipuka, wanasiasa wengi wakuu watahamia UDA kabla ya mchujo wa vyama vya kisiasa,” alisema mbunge wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri.

Mgombeaji wa kiti cha eneobunge la Bureti, Bw Malon Rono anasema kuwa UDA kitashinda viti vingi katika eneo la Rift Valley.

Kulingana na mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, chama hicho kina ufuasi mkubwa Rift Valley ilivyodhihirishwa na umati unaohudhuria mikutano ya Bw Odinga.

“Wale wanaodai kuwa ODM haina wafuasi Rift Valley wanafaa kutazama umati uliomkaribisha Bw Odinga katika ziara zake za majuzi,” alisema Bw Mbadi.

Aliongeza, “Uasin Gishu, Pokot Magharibi, Nakuru na Trans Nzoia, wabaini kwamba tutawashangaza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.”

Hata hivyo, mfanyabiashara wa Nairobi, Bw Alvin Kibet, alisema kwamba chama kitakachowavutia vijana kwa wingi Rift Valley ndicho kitazoa kura nyingi.

You can share this post!

Mudavadi, Weta wajianika kwa kususia hafla ya Raila

Hisia mseto zatolewa kufuatia kauli ya Ngilu...

T L