Habari Mseto

ODM kupigania fidia kwa jamii zote zilizopoteza jamaa

May 6th, 2018 1 min read

Na BARACK ODUOR

KINARA wa upinzani Raila Odinga amewaomba wabunge wa ODM kumsaidia kupitia bungeni kuhakikisha familia zilizopoteza jamaa wao zimefidiwa na serikali.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na mwenzake kutoka Suba kaskazini Bi Millie Odhiambo wamedokeza kuwa Bw Odinga anataka uungwaji mkono kutoka bungeni kuhakikisha sekali imetoa malipo ya fidia kwa waliouawa.

Viongozi hao walisema wanaendelea kuandaa orodha ya idadi kamili ya familia zilizoathiriwa ili kuwasilisha kwa serikali kupitia afisi ya Bw Odinga.

“Tunajua watu wengi wanauliza kuhusu hatima ya waliofariki wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi wa Rais Kenyatta. Sisi tukiwa wabunge kutoka Nyanza tunasukuma suala hili la kufidiwa kwa wahasiriwa,” alisema Bw Amollo.

Wakizungumza wakati wa mazishi ya Mzee Isaac Ooro, baba yake mshauri wa kisiasa wa Bw Odinga, Silas Jakakimba katika kijiji cha Kakimba kisiwani Mfang’ano Jumamosi, wabunge hawa wa walisema watashinikiza hadi wahusika wafaidi kutokana na ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge hawa walisema kuwa lazima haki ipatikane kwa walioathiriwa wakati wa makabiliano hayo kati ya waandamanaji na Polisi.

“Salamu na ushirikiano kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta haujatufanya tusahau maafa yaliyotokea Wakenya wasio na hatia walipouawa na dhuluma nyingine kutekelezwa,” alisema Bw Amollo.

Mbunge huyo pia alisema kuwa maafa na dhuluma za hapo awali lazima zijadiliwe ndipo suluhisho lipatikane.

Bw Amollo alisema kwamba wabunge kutoka eneo hilo wanashirikiana kuhakikisha wafuasi wa NASA waliothiriwa wamepata haki.

“Tuko tayari kuwasilisha majina ya wahasiriwa kwa Serikali na pia mahakamani kuhakikisha haki imetendeka na dhuluma zilizotokana na uchaguzi mkuu zimetatuliwa,” alisema Bw Amollo.