HabariSiasa

ODM kutolewa pumzi ishara ya kufifia kwa 'Baba'

April 7th, 2019 2 min read

CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

LICHA ya kujipiga kifua na kujigamba kuwa ingetwaa ushindi mkubwa katika uchaguzi mdogo wa maeneobunge ya Ugenya na Embakasi Kusini, ODM ilirambishwa sakafu na wagombeaji wa vyama vingine ilivyodharau.

Wakosoaji wa chama hicho walisema kichapo hicho ni ishara ya kufifia kuwa umaarufu wa kiongozi wake Raila Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika matokeo yaliyotangazwa usiku wa kuamkia Jumamosi, Bw David Ochieng’ wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) alitangazwa mbunge mteule wa Ugenya kwa kuzoa kura 18,730 na kumshinda mgombeaji wa ODM, Christopher Karan aliyepata kura 14,507.

Na katika eneobunge la Embakasi Kusini, Bw Mawathe wa chama cha Wiper aliibuka bingwa kwa kuzoa kura 21,628 huku Irshad Sumra wa ODM akipata kura 7,988 pekee.

Kiti kilipotangazwa wazi, ODM ilikataa ombi la Wiper kuiachia kiti hicho na kujigamba kuwa ina umaarufu wa kutosha kushinda.

Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi huo, viongozi wa ODM, wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna walijitanua kifua wakisema kwamba,watapata ushindi kwa urahisi kudhihirisha ubabe wake katika ulingo wa siasa nchini na ndani ya Muungano wa NASA.

Hii, kulingana na wadadisi, ndio iliyopelekea vyama tanzu katika muungano huo, Ford Kenya na ANC, kuamua kuunga mkono Bw Mawathe katika kinyang’anyiro cha Embakasi Kusini.

Mgombeaji huyo wa Wiper pia alipigwa jeki na wabunge wa Jubilee kutoka Kaunti ya Nairobi na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Hii ni licha ya chama hicho tawala kutangaza kuwa hakingekuwa na wagombeaji “ili kutopandisha joto la kisiasa katika kipindi hichi cha handisheki,”

Ushindi wa Ochieng’ umefasiriwa kuwa pigo kwa ODM katika ngome ya kiongozi wake Raila Odinga. Kushindwa kwa chama hicho kulikifanya kuchongolewa na wapinzani wakuu wa Bw Odinga akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Kwenye ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dkt Ruto aliwapongeza washindi akisema wao ni ushindi wa masikini wa kawaida dhidi ya mibabe wa kisiasa na ambao umeletwa na Mungu.

“Pongezi Ochieng (Ugenya) na Mawathe (Embakasi) kwa ushindi wenu ambao umeletwa na Mungu. Huu ni ushindi wa mahasla, uamuzi wa wananchi. Jina la Mungu litukuzwe,” akasema.

Dkt Ruto na wandani wake walisema kubwagwa kwa ODM ni kielelezo cha kudidimia kwa umaarufu wa chama hicho kwa kuendeleza siasa za migawanyiko nchini kwa kumponda naibu rais kila mara.

“ODM waligeuza William Ruto kuwa mada ya kampeni Ugenya na Embakasi. Waliwataja washindani wao kama watu Ruto. Lakini wapiga kura walipuuza hayo na kufanya maamuzi ya busara,” akasema Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.

Naye kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen alisema ushinde wa ODM ni ithibati kuwa juhudi zake za kumwondoa afisini Dkt Ruto kupitia mlango wa nyuma zitaambulia patupu.

Wakati huo huo, chama hicho kimekubali kushindwa na kuwapongeza wagombeaji wake walioshiriki chaguzi hizo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa uchaguzi katika ODM Junet Mohamed alisema uongozi wa chama hicho utachunguza kiini cha kushindwa kwa maeneo ambayo ni ngombe yake.