ODM matumaini tele kuhifadhi ugavana Mombasa

ODM matumaini tele kuhifadhi ugavana Mombasa

VALENTINE OBARA Na KENNEDY KIMANTHI

CHAMA cha ODM katika Kaunti ya Mombasa, kimezidisha matumaini yake ya kuhifadhi kiti cha ugavana baada ya kujizolea viti vitano kati ya sita vya ubunge.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliahirisha uchaguzi wa ugavana Mombasa na Kakamega hadi Agosti 23, baada ya karatasi za kura kupatikana zikiwa na dosari.

Mgombeaji ugavana Mombasa kupitia ODM, Bw Abdulswamad Nassir, alisema matokeo ya uchaguzi wa ubunge, ni dhihirisho kuwa Pwani bado ni ngome ya chama hicho na kinara wake, Bw Raila Odinga.

“Tunaomba wapigakura wetu wajitokeze kwa idadi kubwa ili tupate gavana wa ODM Mombasa katika uchaguzi ulioahirishwa. Msibabaishwe wala kutiwa woga,” akasema Bw Nassir, mwishoni mwa wiki iliyopita.

ODM ilishinda viti vya ubunge Changamwe, Likoni, Kisauni, Mvita na Jomvu mbali na kuhifadhi viti vya useneta na mbunge mwakilishi wa kike.

Hata hivyo, chama hicho kilipata pigo katika eneobunge la Nyali ambapo Bw Mohamed Ali, alifanikiwa kuhifadhi kiti chake kupitia Chama cha UDA. Bw Said Abdalla, wa Chama cha ODM, aliibuka wa pili.

Vilevile, matokeo ya kura za urais Pwani pia yaliashiria Dkt William Ruto, alipata kura nyingi eneobunge la Nyali ikilinganishwa na maeneobunge mengine mengi ukanda huo.

Kwa mujibu wa takwimu za IEBC, Dkt Ruto alipata kura 23,613 huku mgombeaji urais kwa tiketi ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Odinga, akiongoza kwa kura 31,717 katika eneobunge hilo.

Dkt Ruto alionekana pia kutoa ushindani mkali dhidi ya Bw Odinga katika maeneobunge ya Kisauni na Changamwe kwa kuzoa kura 22,098 na 19,098 mtawalia.

Bw Odinga alipata kura 35,383 Kisauni na 24,237 Changamwe, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na IEBC.

Baada ya kutangazwa mshindi, Bw Ali alitoa wito kwa wapinzani wake kushirikiana naye kwa manufaa ya wakazi wa Nyali.

“Ilikuwa ni uchaguzi mgumu na rahisi wakati huo huo. Ulikuwa mgumu kwa sababu niliugua katika kipindi cha uchaguzi, na rahisi kwa sababu watu wa Nyali walisimamia ukweli wakaniunga mkono,” akasema.

Katika eneo la Pwani, ODM tayari imefanikiwa kuhifadhi kiti cha ugavana Kaunti ya Kilifi na Tana River licha ya ushindani mkali kutoka kwa UDA.

Bw Gideon Mung’aro, alitangazwa mshindi wa kiti hicho Kilifi alipombwaga Bi Aisha Jumwa, ambaye aliwania kupitia kwa UDA kilicho ndani ya Muungano wa Kenya Kwanza.

Gavana Dhadho Godhana, alifanikiwa kuhifadhi kiti chake kwa awamu ya pili Tana River kupitia Chama cha ODM, na kumshinda kwa karibu aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, Bw Hussein Dado (UDA).Chama cha UDA kilipata kiti kimoja pekee cha ugavana Pwani, katika Kaunti ya Kwale, ambapo Bi Fatuma Achani alitangazwa mshindi.

Bi Achani alikuwa naibu wa Bw Salim Mvurya, kupitia Chama cha Jubilee 2017.

Ugavana Lamu uliendea Bw Issa Timamy (ANC), huku Bw Andrew Mwadime, akishinda akiwa mgombeaji huru Taita Taveta.

  • Tags

You can share this post!

Ndiritu Muriithi aisuta IEBC kwa kuwafungia nje ya Bomas

WANTO WARUI: Wazazi washirikishwe katika uchaguzi wa shule...

T L