ODM motoni kuacha Maitha katika mataa

ODM motoni kuacha Maitha katika mataa

VALENTINE OBARA NA WACHIRA MWANGI

SIASA si hasa, ni msemo ambao hutumiwa na wengi kuashiria jinsi ulingo wa siasa unavyogeuka na kupinduka huku na kule kila kukicha.

Kwa baadhi ya wanasiasa, msemo huu umedhihirika sana katika matukio yanayoendelea kushuhudiwa wakati mipango inazidi kusukwa kuelekea kwa uchaguzi wa Agosti.

Katika Kaunti ya Mombasa, mmoja wa wanasiasa ambao pengine wameona ukweli wa msemo huu mapema mno kabla hata kujitosa kikamilifu ulingoni, ni Bi Selina Maitha, ambaye ni dada ya aliyekuwa mbunge wa Kisauni, marehemu Karisa Maitha.

Miezi michache iliyopita, Bi Maitha aliungana na mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal, wakitaka tikiti ya ODM kuwania kiti cha Gavana Hassan Joho.

Bi Maitha alikuwa amejiuzulu kutoka serikalini ambapo alikuwa akihudumu kama naibu kamishna katika Kaunti ya Machakos.

Wakati ilipobainika kuwa Bw Shahbal alikubali uamuzi wa ODM kumpa Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, tikiti ya moja kwa moja kwa ugavana Mombasa, Bi Maitha alikuwa mmoja wa wale waliomsihi kujitosa uchaguzini kama mgombea huru.

Hata hivyo, Bw Shahbal alikataa wito huo na hatimaye Bi Maitha akaamua kujiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambapo atakuwa mgombea mwenza wa ugavana wa seneta wa zamani, Bw Hassan Omar.

Mdahalo kuhusu hatima ya Bi Maitha uliibuka upya wikendi, wakati Bw Omar alipodai kitendo alichofanyiwa kilikuwa cha udhalimu.

Bw Omar alisema Bi Maitha alishawishika kujiuzulu kazi yake serikalini akijua atakuwa mgombea mwenza wa ugavana Mombasa, kisha baadaye akaachwa kwa mataa.

“Gavana Joho alimtema aliyekuwa naibu wake, Bi Hazel Katana baada ya kushinda ugavana 2013. Alipoingia 2017 alikuwa na Dkt William Kingi ambaye ni msomi lakini pia yeye akatengwa. Hivi majuzi, rafiki yake, Bw Suleiman Shahbal, alimtema Bi Maitha baada yake kujiuzulu kutoka kwa kazi yake kwa sababu za kibinafsi,” akasema Bw Omar.

Alikuwa akizungumza katika hafla ya kupokea azimio la sehemu ya jamii ya Wamijikenda iliyofanywa Majaoni, Kaunti ya Mombasa mnamo Jumamosi.

Kwa upande wake, Bi Maitha alisisitiza kuwa nia yake kujiunga na siasa ilikuwa kwa lengo la kuchangia mabadiliko katika maisha ya wakazi wa Mombasa.

Kulingana naye, kumekuwa na pengo kubwa la kutetea maslahi ya Wamijikenda hasa Mombasa tangu kakake alipofariki miaka 18 iliyopita.

“Tutakomboa Mombasa tu iwapo tutazungumza kwa sauti moja. Wale ambao wamesimamia kaunti hii kwa miaka kumi iliyopita wamekosea wakazi na hata wale wanaotaka kuwarithi katika uchaguzi wa mwaka huu hawana chochote kipya watakacholeta,” akasema.

Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, alisema jamii ya Wamijikenda hukosa sauti kutokana na mgawanyiko wao kisiasa.

Kulingana naye, UDA ikiongozwa na Naibu Rais William Ruto, imeonyesha nia ya kusuluhisha changamoto ambazo zimekumba Pwani kwa miongo mingi.

Bw Nyonga Makemba, akiongoza wanajamii wenzake alisema wanataka UDA ikishinda itatue suala la ardhi kwa siku 100 za kwanza mamlakani.

Walitaka pia ufufuzi wa viwanda na sekta nyingine zitakazosaidia wakazi moja kwa moja, kama vile utalii, kilimo cha nazi na korosho, uvuvi, uchimbaji madini miongoni mwa mengine.

“Tunataka kujua mna mpango gani kwa manufaa ya jamii ya Wamijikenda katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa iwapo mtashinda. Hatutaki tena kutumiwa tu kuongeza wanasiasa kura,” akasema Bw Makemba.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, na mwenzake wa Lungalunga, Bw Khatib Mwashetani.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi kukamatwa kwa kuficha watoto wahalifu

Saburi akubali kuunga mkono Mung’aro kwa ugavana Kilifi

T L