Habari Mseto

ODM wahisi upweke kufuatia Joho kushika shughuli zake

February 1st, 2024 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WANACHAMA wa ODM wanaendelea kusononeka kuhusiana na kutokuwepo kwa naibu kiongozi ambaye pia alikuwa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho kwenye shughuli ya kusaka wanachama wapya.

Bw Joho alikuwa na ushawishi mkubwa katika ODM sawia na kuwa na umaarufu mkubwa eneo la Pwani hata kutambulika kama sultani wa Pwani.

Hata hivyo tangu kufifia kwake katika chama cha ODM, wanachama hao hasa kaunti ya Mombasa wamekuwa wakikosa mwelekeo huku vita baina ya viongozi na wanasiasa vikiendelea kudhihirika.

Wakiongozwa na aliyekuwa mwakilishi wa wadi ya Tudor, Bw Tobias Samba, viongozi hao walisema kutokuwepo kwa Bw Joho kushiriki kikamilifu katika chama hicho kumedhohofisha ODM.

“Kutokuwa kwa Gavana Joho kwenye siasa za chama kumetuathiri pakubwa. Wakati Joho alikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa eneo la Pwani. Alikuwa anatoa maagizo na tunafuata. Tunamuomba atoke likizoni,” alisema aliyekuwa mwakilishi wa wadi ya Tudor, Bw Tobias Samba.

Alisema huenda Bw Joho aliondoka kwenye siasa za chama baada ya Bw Odinga kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Hata hivyo amemtaka arudi ulingoni.

“Rudi uchukue usukani tutakufuata,” aliongeza.

Bw Samba amewashtumu viongozi wa ODM kwa kuwatenga wakati wa shugli za kuwasajili wanachama wapya.

“Tunataka safari hii uchaguzi wa wakuu wa chama cha ODM kaunti ya Mombasa ufanyike. Wakati wa mwisho chama chetu kiliandaa uchaguzi wa wakuu chama ilikuwa ni wakati marehemu Bw Ramadhan Kajembe na Mohammed Hatimy,” alisema.

Baadaye, ODM ikamchagua Bw Mohammed Khamis ambaye ana ukoo na familia ya Bw Joho kama mwenyekiti.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wanasema ameshindwa kuongoza chama vyema.

“Wakati Dee amekuwa mwenyekiti tumeona chama chetu kikianza kufifia hasa katika uongozi ndio maana nimejitokeza kuwania kiti hiki cha uwenyekiti ili niimarishe chama chetu,” alisema.

Bw Samba alisema chama hicho kina viongozi ambao wanajihusisha na maswala ya ODM wakati kinara wao Bw Raila Odinga anatua Mombasa.

“Lakini Bw Odinga akiondoka kunakuwa na kimya. Lakini tunataka kubadilisha ODM,” aliongeza.