ODM: Wanaotafuta ugavana wajitokeze

ODM: Wanaotafuta ugavana wajitokeze

Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha ODM katika kaunti ya Kilifi kimewataka wagombea viti vya ugavana katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kujitokeza na kutangaza azimio lao kwa umma.

Chama hicho kilionya kuwa hakitaki watu wanaotafuta kiti cha ugavana kwa dhihaka.

Kwa sasa chama cha ODM kina wagombeaji wanne wanaotaka kumrithi gavana Amason Kingi anayehudumu kupindi chake cha mwisho baada ya kuchaguliwa mwaka wa 2013.

Wagombea hao ni waziri mdogo wa ugatuzi Bw Gideon Mung’aro, naibu wa Gavana wa kaunti ya Kilifi Bw Gideon Saburi, spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Bw Jimmy Kahindi na balozi wa Kenya nchini Tanzania Bw Dan Kazungu.

Bw Mung’aro anayesemekana kuwa anayetakiwa na wakuu wa ODM, alirudi katika chama hicho baada ya kukitoroka mwaka 2016 na kujiunga na Jubilee.

Kwa upande wake Bw Saburi na Bw Kazungu ni wanachama daima wa chama cha ODM huku spika Kahindi akiwa alikuwa hana chama bali kulikuwa na tetesi kuwa angewakilisha chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Bw Kazungu alikuwa mbunge wa Malindi kabla ya kuteuliwa na serikali ya Jubilee kuwa waziri wa Madini.

Baadaye aliteuliwa kuwa balozi.

Akizungumza na wanahabari katika shule ya msingi ya Mwarandinda katika wadi ya Sokoke, eneobunge la Ganze, mwenyekiti wa ODM kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alisema kuwa ni muhimu kwa wagombea viti hao kujitokeza nyanjani ili waweze kujulikana.

“Nawasihi wale wanne wajitokeze ili waweze kujulikana na pia kuweka mikakati. Kwa sasa mambo yanaendelea na hakutakuwa na wakati kufikia mwezi Aprili wakati wa mchujo. Kama mtu hatakuwa amesajili wanachama wengi, asije akalia akisema kuwa kura zake zimekuwa chache,” akasema.

Alisema kwa sasa chama cha ODM kinaendelea kupokea wanachama waliokuwa wamekiasi na pia wanachama wapya.

“Cha msingi kwetu ni kuweka mikakati kuhakikisha kura za mchujo zitakuwa ni za haki, wazi na kila mwanachama ataruhusiwa kushiriki. Haitawezekana tena kuwa mtu ambaye yuko chama cha Jubilee kufanya mchujo wa chama cha ODM. Kila mtu atabaki kule yuko,” akasema.

Alitoa witu kwa wanachama wote ambao wananuia kugombea viti mbalimbali, wasajili wanachama wengi ili waweze kuwachagua ifikapo kura ya mchujo.

Bw Mwambire alidokeza kuwa kwa sasa chama cha ODM bado kinaendelea kujipanga, na kwamba ushirikiano na vyama vingine haumaanishi kuwa chama cha ODM kitavunjwa ama kitatupilia mbali msimamo wake kisiasa.

“Chama cha ODM kiko imara na sisi hatutaweza kuachilia nafasi yoyote,” akasema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa ana imani kuwa sheria kuhusu miungano ya vyama itazingatia miungano ya vyama katika ngazi ya kitaifa.

“Nina imani kuwa sheria muungano utabaki huko juu peke yake lakini huko chini tutabaki kung’ang’ania hivi viti kwa vyama vyetu,” akasema Bw Mwambire.

Kwa upande wake Bw Mung’aro alisema kuwa anaendeleza kampeni zake mashinani kwa utaratibu ila hafanyi kwa kasi kwa sababu msimu wa kampeni haujaanza rasmi.

“Niko mashinani sana na nimejulikana kila sehemu ya kaunti ya Kilifi,na sifanyi kampeni kwa fujo kwa sababu mwaka wa uchaguzi bado,” akasema.

Alisema kuwa ana imani anatosha kumrithi Kingi kwa sababu ya historia yake ya utendaji kazi bora katika kaunti ya Kilifi na serikali kuu.

You can share this post!

Wahamiaji 27 wafa maji Pwani ya Libya

Mawakili wanaounga pande kinzani mfano wa siasa safi!

T L