HabariSiasa

ODM wapinga noti mpya

June 3rd, 2019 2 min read

RUTH MBULA na MARY WAMBUI

VIONGOZI wakuu wa Chama cha ODM, wamepinga noti mpya zilizozinduliwa na Benki Kuu ya Kenya mnamo Jumamosi, na kusema zinakiuka katiba kwa hivyo hazifai kuanza kutumiwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw John Mbadi alisema ingawa wanaunga mkono lengo la Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi kwa kuondoa noti za sasa, hasa za Sh1,000 katika matumizi, hawataogopa kumwambia waziwazi kuhusu ukiukaji wa katiba kwa kujumuisha sura ya aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hili, Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

“Hatuwezi kuruhusu ukiukaji wa katiba ambayo iko wazi kwamba noti mpya hazifai kuwa na sura ya binadamu yeyote. Ni wazi kwamba kuna mtu alitumia ujanja kuingiza sura ya marehemu rais (Jomo Kenyatta),” akasema Bw Mbadi.

Kwenye noti hizo ambazo Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK), Dkt Patrick Njoroge alisema zinaonyesha sura ya sekta muhimu za taifa, kuna picha ya Jumba la KICC iliyojumuisha sanamu ya Mzee Kenyatta ambayo huwa iko nje ya jumba hilo.

Sekta zilizowakilishwa katika noti hizo za kuanzia Sh50 hadi Sh1,000 ni kawi safi, kilimo, huduma za kijamii, utalii na utawala bora.

“KICC ni jumba kuu. Inafaa watafute upande wa jumba hilo ambao hauna sura ya binadamu yeyote,” akasema Bw Mbadi, ambaye pia ni Mbunge wa Suba Kusini na Kiongozi wa Wachache Bungeni.

Kauli yake iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna pamoja na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo aliye pia Kiongozi wa Wachache katika Seneti na mwandani mkubwa wa Kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga.

Walizungumza katika eneo la Rongo, Kaunti ya Migori walipoongoza harambe ya kanisa la St Martin De Pore.

“Kuna Wakenya wanaoweza kwenda mahakamani kupinga noti hizo mpya. Watauliza kwa nini kuna sura ya binadamu. Mimi nikiwa wakili, sitanyamaza. Isitoshe, nitakuwa hatarini nikinyamaza endapo kesi aina hii itawasilishwa kortini,” akasema Bw Orengo, akimwomba Rais Kenyatta afuate matakwa ya kikatiba.

Dkt Njoroge alikuwa ametangaza noti za sasa za Sh1,000 zitaacha kutumiwa Oktoba 1, kwani hazitakuwa halali kuanzia wakati huo.

Tangazo hilo lilionekana kulenga mabwanyenye ambao inaaminika huficha mabunda ya fedha manyumbani mwao ili kuepuka kulipa ushuru, au kuepuka kuadhibiwa kisheria kwa kupata fedha hizo kwa njia haramu.

Jana, wandani wa Naibu Rais William Ruto wanaofahamika kama ‘Team Tangatanga’, walipuuzilia mbali taswira inayoenezwa na baadhi ya wananchi kwamba wao ndio walilengwa na agizo hilo ikizingatiwa desturi yao ya kuchangisha mamilioni ya fedha makanisani karibu kila wikendi.

“Baadhi ya watu tayari wameingiza siasa katika agizo hilo, wakisema tumeficha pesa katika magunia manyumbani mwetu. Tunataka muda wa kuharamisha noti hizo kufupishwa kuwa miezi miwili, ili wakituona tukiendelea kuhudhuria harambee baada ya miezi hiyo miwili wakose cha kusema,” mbunge wa Lang’ata Nixon Korir alisema walipokuwa Kiambu.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, pia alipendekeza muda wa kuharamisha noti hizo ufupishwe ndipo matapeli wanaswe kwa urahisi zaidi.