ODM yaacha vyama vidogo jangwani

ODM yaacha vyama vidogo jangwani

Na RUSHDIE OUDIA

CHAMA cha ODM, kimejiondoa katika mazungumzo yaliyolenga kuungana na vyama vidogo vya kisiasa katika ngome yake ya Nyanza, kikisisitiza kwamba kinataka wagombeaji wake katika nyadhifa zote sita kuchaguliwa, ili kipate nguvu katika bunge la kitaifa na mabunge ya kaunti baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, kinasema kwamba kitazungumzia suala la muungano na vyama nje ya ngome zake.

Hatua hiyo inajiri kukiwa na malalamishi kwamba kuna wagombeaji wanaopendelewa kwa viti tofauti na shinikizo kutoka kwa Bw Odinga wawaniaji wakubaliane miongoni mwao ili kuzuia mgawanyiko unaoweza kufaidi vyama vidogo.

Japo kunaweza kuwa na sababu halisi kuhusu wasiwasi wa mchujo wa chama kufanya baadhi ya wanasiasa kutafuta tiketi za vyama vingine, chama cha ODM kinasisitiza kuwa wanaounga azma ya urais ya Bw Odinga, hawana budi ila kujiunga na chama chake kuweza kugombea viti vingine.

Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, alisema yeye binafsi, anajaribu kuzungumza na mbunge wa Ugenya, Bw David Ochieng ambaye ni kiongozi wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG).

“Tunataka kuwa na idadi kubwa ya wanachama katika mabunge yote mawili na katika mabunge ya kaunti. Tunazungumza na vyama vilivyo na maono sawa na yetu nje ya Nyanza,” alisema Bw Mbadi.

Bw Mbadi aliambia Taifa Leo kwamba baadhi ya vyama vidogo vinachukuliwa kuwa vya kuharibu hesabu na kwa hivyo, hawatazungumza navyo, akitaja mfano wa chama cha People Democratic Party (PDP) cha Gavana wa Migori, Okoth Obado.

Alidai kwamba anachotaka Bw Obado ni kutafuta kudumu katika siasa baada ya kukamilisha muhula wake wa pili kama gavana.

Bw Obado na vyama vingine eneo la Nyanza, amekuwa akishinikizwa kuacha azma yake na kuunga azma ya urais ya Bw Odinga katika juhudi za kuhakikisha kuwa eneo hilo litapiga kura likiwa limeungana kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Huku wanasiasa walio na vyama vidogo wakisema watasimamisha wagombeaji katika nyadhifa za udiwani hadi ugavana, ni Bw Obado pekee ambaye ametangaza kuwa chama chake cha PDP kitakuwa na mgombea urais wake.

Gavana huyo hakuhudhuria mikutano ya kampeni ya Naibu Rais William Ruto katika eneo la Kuria Jumapili iliyopita, ishara kuwa huenda amebadilisha mpango wa chama chake kushirikiana na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mkurugenzi wa masuala ya siasa wa ODM Opiyo Wandayi, pia alisisitiza kuwa chama hicho hakitazungumza na vyama vidogo lakini akaongeza hakuna anayezuiwa kuunga azma ya urais ya Bw Odinga.

Baadhi ya vyama vidogo katika eneo la nyanza ni PDP cha Bw Obado, MDG cha Bw Ochieng, United Green Movement kinachoongozwa na aliyekuwa mbunge wa Ndhiwa Agustino Neto na Green Congress Party of Kenya kinachohusishwa na Bw Martin Ogindo.

  • Tags

You can share this post!

AFCON: Ivory Coast wakung’uta Equatorial Guinea...

Ruto aambia wapinzani waache vitisho

T L