Habari

ODM yadai kunyimwa pesa kwa kususia kura 2017

November 18th, 2020 1 min read

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kimedai kuwa kilinyimwa fedha na msajili wa vyama vya kisiasa, kwa kuwa kiongozi wa chama hicho Raila Odinga alisusia marudio ya uchaguzi wa urais mwaka wa 2017.

Baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Muungano wa NASA ulikataa kushiriki marudio ya uchaguzi huo Oktoba, kwa madai kuwa Tume ya Uchaguzi (IEBC) haikuwa na uwezo wa kusimamia uchaguzi wa kweli na haki bila kufanyiwa mabadiliko.

NASA ilijumuisha ODM pamoja na Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka, Amani National Congress (ANC) ya Musalia Mudavadi na Ford Kenya ya Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, Jumanne alimlaumu msajili wa vyama vya kisiasa, Bi Anne Nderitu, kwa kukataa kukabidhi chama hicho mamilioni ya fedha inavyohitajika kisheria.

“Inafahamika wazi kuwa Mahakama ya Juu ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017. Ni kwa msingi huu ambapo msajili wa vyama vya kisiasa husema hawezi kuzingatia matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, 2017 kutoa fedha za kufadhili vyama vya kisiasa. Kwa mtazamo wetu, msimamo wake unakiuka sheria,” akasema.

Katibu huyo alikuwa akirejelea malalamishi yaliyoibuka upya kutoka kwa vyama tanzu vya NASA kwamba ODM imekataa kuvigawia fedha kutoka kwa afisi ya msajili wa vyama.

Bw Sifuna alisema chama hicho kimewasilisha malalamishi mara kadhaa kwa msajili wa vyama kuhusu msimamo wake ambao umechangia Jubilee pekee kufadhiliwa na fedha za umma, lakini lalama zao hazitiliwi maanani.

“Tumemtaka hata aende kwa Mahakama ya Juu ili kupata ufafanuzi kuhusu hatua anayofaa kuchukua kutoa fedha za vyama lakini hataki kufanya hivyo,” akasema.

Alimtaka Bi Nderitu awe akieleza wazi masuala hayo kila wakati malalamishi yanapoibuka, huku akitaka pia vyama vinavyodai kunyimwa fedha na ODM vitafute ushauri wa kisheria.