ODM yaenda kortini kupinga matokeo ya kura za Matungu

ODM yaenda kortini kupinga matokeo ya kura za Matungu

Na JOSEPH WANGUI

UHASAMA kati ya vyama viwili vya Amani National Congress (ANC) na Orange Democratic Movement (ODM), sasa umeelekezwa mahakamani.

Hii ni baada ya ODM kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Matungu uliofanyika Machi 4, 2021.

Katika kesi hiyo, aliyekuwa mgombea wa ODM, David Were, amedai kuwa maajenti wa ANC pamoja na maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) walikiuka sheria kadhaa, hali iliyomsaidia mgombea Peter Oscar Nabulindo kunyakua ushindi.

Kupitia Marende & Nyaundi Associates, Bw Were anadai kuwa IEBC ilikuwa na ubaguzi kwa sababu maajenti wa ODM hawakuruhusiwa kushiriki wala kushuhudia kufunguliwa na kufungwa kwa masanduku ya kura na hata kuhesabu kura katika baadhi ya maeneo.

Anadai kuwa maajenti wake walifukuzwa wakati wa kuhesabu kura, ambapo nakala kadhaa za Fomu 35A hazikutiwa sahihi na majenti wa ODM na hakuna ufafanuzi wowote

Bw Were ananuia kuthibitisha madai yake kwa kutumia mashahidi sita ambao pia wameandikisha hati za kiapo.

Nakala hizo zinasema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya ukatili na vitisho dhidi ya maajenti wa Bw Were na maafisa wa IEBC.

Anafafanua kuwa dhuluma walizopitia maajenti na wafuasi wake ni pamoja na kutekwa nyara, kuchapwa na kujeruhiwa, kudungwa kisu, kufyatuliwa risasi, kukimbizwa, maafisa na maajenti kuandamwa manyumbani kwao na kushambuliwa kikatili siku ya uchaguzi.

Mashaka mengine ni pamoja na kukemewa na kunyooshewa vidole kwa maafisa wa IEBC waliokuwa wamesimamia shughuli hiyo, maajenti, maafisa na wafuasi wa ODM kutishiwa maisha ndani na nje ya vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi huo.

“Mafisa wa IEBC, maajenti wa mlalamishi na maafisa wa chama walifyatuliwa risasi, kudungwa kisu, kuchapwa na kucharazwa. Kwa mfano, Seneta Cleophas Malala aliwatishia na kuwashambulia wapigakura na maafisa wasimamizi katika vituo vya kura vya Munami, Mayoni, Mwira, Emakale, Namayiakalo na Emanani miongoni mwa vingine,” inasema nakala hiyo.

You can share this post!

Tineja adaiwa kumuua na kumkata kichwa nyanya yake

Uhuru ashauriwa kuiga Kibaki