ODM yakana madai Raila anatakasa mafisadi

ODM yakana madai Raila anatakasa mafisadi

Na ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha ODM kimekanusha madai kuwa kinashirikiana na watu ambao wameshtakiwa kwa ufisadi hivyo kuhujumu juhudi za serikali za kukomesha uovu huo.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mwenyekiti wa Orange Democratic Movement (ODM) John Mbadi, na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, walishutumu wabunge wa mrengo wa Tangatanga wanaomuunga Naibu Rais William Ruto, kwa kutumia jina la chama hicho kama kisingizio cha kuelezea kutamaushwa kwao na Rais Uhuru Kenyatta ambaye amekosa kuwasikiza.

Bw Mbadi, ambaye pia ni Kiongozi wa Wachache Bungeni amempuuzilia mbali Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na wenzake.

Wakati wa kikao kuhusu iwapo wamshurutishe Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kujitetea mbele ya kamati maalumu au kikao kamili cha seneti, seneta huyo alidai afisi ya Capitol Hill ya aliyekuwa Waziri Mkuu, imegeuzwa kituo cha kunadhifisha ufisadi.

Mbunge huyo wa Suba Kusini alijitokeza vikali akisema ODM kamwe haiungi mkono wala kumtetea yeyote aliyeshutumiwa kwa ufisadi.

“Kilichotokea wiki iliyopita wakati wa kikao kuhusu kumfurusha Gavana Waiguru kinaashiria kuwa maseneta wa Tangatanga wana hasira, machungu na wamekata tamaa kwa sababu Rais hawatilii maanani tena,” alisema Bw Mbadi.

Kuhusu madai kwamba, baadhi ya magavana wa ODM wanafuja raslimali za umma na hawajawahi kuhojiwa, mbunge huyo alitetea ODM akisema chama hicho si tume ya uchunguzi wala mashtaka, hivyo basi madai hayo hayana msingi na yanatokana na kisasi cha siasa.

Alihoji kuwa iwapo chama hicho kilikuwa kikishirikiana na watu wafisadi, baadhi ya viongozi wa kaunti wanaohojiwa kwa madai ya ufisadi, hawangekuwa wakipitia mchakato huo.

Mbunge huyo alisema, Rais Kenyatta na Bw Raila Odinga wamejitolea kuhakikisha ufisadi nchini umeangamizwa.

Alieleza kuwa iwapo ODM ilikuwa ikiwalinda viongozi wafisadi, Gavana wa Busia Sospeter Ojamong na aliyekuwa gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero hawangeshtakiwa.

“Rais na kiongozi wa ODM wanaamini ufisadi umekuwa suala sugu nchini na ni sharti ukabiliwe kwa manufaa ya raia wa Kenya,” alisema Bw Mbadi.

Aidha, alisema madai ya wandani wa Naibu Rais kwamba, kamati haitawatendea haki wakazi wa Kirinyaga hayakuwa na msingi.

“Kamati inayodadisi utendakazi wa Bi Waiguru ni miongoni mwa njia bora zaidi zilizojikita katika sheria zetu. Itapatia pande zote mbili muda wa kutosha kusikizwa kushinda kikao mahsusi kitakachochukua muda mrefu ikilinganishwa na kamati itakayochukua angalau siku tatu,”

“Seneta Kipchumba Murkomen na kundi lake ni wanafiki wanaotaka kujihusisha na sarakasi,” alisema Bw Mbadi akiongeza kuwa ODM haijatoa taarifa rasmi itakayomnusuru gavana huyo anayepigwa vita.

Kama kawaida, maseneta wanaoegemea Naibu Rais walikataa mswada huo na kuupinga vikali lakini hawakufanikiwa huku upande wa wengi ukiwabwaga.

Waliongozwa na maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) John Kinyua (Laikipia), Mithika Linturi (Meru) Aaron Cheruiyot (Kericho), Susan Kihika (Nakuru), Christopher Langat (Bomet), wote waliopiga kura kupinga mchakato wa kamati ya bunge kusikiza shutuma hizo.

You can share this post!

Serikali yakiri corona inachangia mimba za mapema

Raila hajaenda ng’ambo kwa matibabu – ODM

adminleo