ODM yakana Oparanya aelekea kwa Ruto

ODM yakana Oparanya aelekea kwa Ruto

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM, kimekanusha ripoti kwamba naibu kiongozi wake, Bw Wycliffe Ambetsa Oparanya amekisaliti na anapanga kukihama kujiunga na vuguvugu la Hasla la Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Wandani wa Dkt Ruto walinukuliwa na gazeti moja la humu nchini wakidai kwamba Bw Oparanya amekuwa akizungumza na Dkt Ruto kwa muda mrefu hata kabla ya mkutano wa wiki mbili zilizopita katika Kaunti ya Narok kujadili ushirikiano wao kisiasa.

Kwenye taarifa jana, chama hicho kilipuuza madai hayo na kumtetea vikali kikisema kwamba Oparanya, ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, ni mwanachama mwaminifu na mfuasi sugu wa kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

“Oparanya si msaliti kama baadhi ya watu wanavyotaka iaminiwe. Wakati mwingine katika siasa, ni vizuri kusoma yale ambayo mpinzani wako anapanga ili uweze kujiandaa kumkabili,” ODM ilisema katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Philip Etale.

Chama hicho kilikiri kwamba Bw Oparanya alikuwa amekutana mara kadhaa na Dkt Ruto hata kabla ya mkutano wao wa Narok na kwamba kila wakati aliwafahamisha viongozi wake.

“Katika mikutano yake yote, Oparanya amekuwa akifahamisha viongozi wa ODM, akiwemo kiongozi wa chama kuhusu yote aliyojadili na Dkt Ruto,” alisema Bw Etale.

Baada ya mkutano wake na Dkt Ruto katika eneo la Narok, Bw Oparanya alikutana na Bw Odinga na kusema kwamba alimfahamisha waliyojadili.

“ Kwa hivyo, wanachama wa ODM na wafuasi wetu hawafai kufikiri kuna njama katika mikutano anayofanya na Naibu Rais,” alisema.

Kwenye mahojiano ya runinga ya Citizen mnamo Alhamisi, Dkt Ruto alisema amekutana na Bw Oparanya takriban mara tano kujadili wanavyoweza kushirikiana katika vuguvugu la hasla.

“Tumejadili jinsi tunavyoweza kushirikiana pamoja na anavyofurahishwa na kampeni ya hasla na kusaidia masikini kujiinua kiuchumi,” Dkt Ruto alisema.

Hii ni licha ya Bw Oparanya kudai kwamba mkutano wao wa Narok haukuwa umepangwa. Baadhi ya washirika wa Dkt Ruto akiwemo mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua, wamenukuliwa wakisema kwamba Bw Oparanya yuko njiani kuungana kisiasa na Dkt Ruto.

Kulingana na Bw Gachagua, ni gavana huyo aliyekuwa wa kwanza kuomba ajiunge na vuguvugu la hasla.

Hata hivyo, taarifa ya ODM iliashiria kwamba alikuwa ametumwa na chama hicho kudadisi mipango ya Dkt Ruto.

“Nataka kusema kwamba ni kweli Bw Oparanya amefanya mikutano michache na Naibu Rais William Samoei Ruto, iwe ni Nairobi au kwingine na kama alivyosema Mahatma Gandhi “unapokabiliwa na adui, mshinde kwa kumuonyesha upendo”, wakati mwingine ni muhimu kusoma mpinzani wako anayopanga uweze kujiandaa vyema kumkabili,” ilisema taarifa ya chama hicho cha chungwa.

Mnamo Ijumaa, Dkt Ruto alisema anamchukulia Bw Odinga kama mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa urais wa 2022. Bw Oparanya mmoja wa wanaomezea tiketi ya urais ya chama cha ODM kwenye uchaguzi huo.

You can share this post!

Serikali yasema haijui walikoenda watahiniwa 12,000 wa KCPE

Nairobi Expressway kutatiza usafiri hadi 2022