Habari

ODM yakana Raila ana mkataba wa siri na Kalonzo

July 27th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM), kimekanusha kwamba kiongozi wake Raila Odinga ana mkataba wa siri na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye mahojiano na gazeti la Sunday Nation, Kalonzo alidai kwamba licha ya muungano wa NASA kusambaratika na chama chake kuamua kuungana na Jubilee, ana mkataba wa siri na Bw Odinga, ambao hawakuhusisha vinara wengine wa muungano huo, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress ANC na Moses Wetangula wa Ford Kenya.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna alitaja kauli ya Bw Kalonzo kama ndoto ya mchana.

“Tumeshangazwa na madai yaliyotolewa na Mheshimiwa Stephen Kalonzo Musyoka kwamba ana mkataba wa siri kati yake na kiongozi wa chama chetu Mheshimiwa Raila Odinga. Tunataka kusema wazi kwamba hakuna mkataba kama huo,” Bw Sifuna alisema kwenye taarifa.

Alisema ni kawaida ya Bw Kalonzo kutaka kuvuna asikopanda na kunufaika na juhudi za watu wengine.

“Tunajua kwamba katika mkataba wa NASA, Bw Kalonzo alijaribu kumsukuma Bw Odinga kumuunga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 lakini kama chama, tulikataa. Hii ndio sababu mkataba wa muungano huo uliachia chama kuunga mshirika yeyote iwapo muungano huo ungedumu 2022. Kauli kwamba kuna mkataba ni ndoto za Kalonzo,” alisema Bw Sifuna.

Katika mahojiano yake na Sunday Nation, Bw Kalonzo alisema kwamba hakuna kipengele kinachohitaji ODM kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa kuwa nilikuwa mgombea mwenza Bw Odinga (kwenye uchaguzi mkuu wa 2017), sitarajii ODM itaniunga mkono 2022. Hata hivyo, nina mkataba binafsi na Bw Odinga ambao washirika wengine katika muungano huo hawahusiki,” alisema na kukataa kufafanua zaidi.

Alikariri kwamba chama chake kiliamua kuungana na Jubilee baada ya NASA kusambaratika na akalaumu ODM kwa kuua muungano huo ili isigawie washirika wake pesa kutoka hazina ya vyama vya kisiasa.

Hata hivyo, Bw Sifuna alisema ODM ilikataa kugawa pesa hizo kwa sababu kilisimamia shughuli za ofisi ya NASA baada ya vyama vingine tanzu kukataza wabunge wake kuchanga Sh10,000 kwa mwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Bw Sifuna alisisitiza kwamba muungano wa NASA ulivunjika Bw Kalonzo, Wetangula na Mudavadi, walipokataa kuhudhuria sherehe ya Bw Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi Uhuru Park mnamo Januari 30, 2018.

“Hao waliua NASA peke yao,” alisema.

Alikanusha madai ya Bw Kalonzo kwamba chama cha ODM kilichangia kuvunjika kwa muungano huo kwa kususia mikutano ya kamati tekelezi akisema ni wawakilishi wa vyama vingine waliohepa.

“ODM na Raila Odinga haina deni la Kalonzo,” alisema Bw Sifuna.

Alisema kwa kuungana na Jubilee, Kalonzo anataka kinga kutoka kwa magavana wa kaunti tatu za ngome yake ya Ukambani Charity Ngilu (Kitui), Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua wa Machakos, ambao wameungana kumpiga vita.

Alikitaka chama cha Jubilee kutomwamini Bw Kalonzo akidai makamu rais huyo wa zamani huwa anatumia miungano ya kisiasa kujifaidi pamoja na wandani wake.