Habari Mseto

ODM yakanusha madai Raila amesaliti Pwani

August 1st, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMUEL OWINO

CHAMA cha ODM kimekana madai ya wabunge wa ‘Tangatanga’ kutoka Pwani kwamba kiongozi wake Raila Odinga amesaliti eneo hilo kwa kupendelea mfumo wa ugavi wa rasilimali unaopokonya eneo hilo fedha.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho Philip Etale, Ijumaa alisema wito wa Bw Odinga kwa maseneta ulikuwa kwamba waupitishe mfumo huo uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kwanza kabla ya kaunti kuongezewa fedha katiba itakaporekebishwa karibuni.

“Raila alitaka mvutano huo umalizwe, kaunti zipate pesa, kisha mapendekezo ya BBI yakipitishwa kaunti zitengewe asilimia 35 ya mapato ambapo kaunti zote zingetengewa fedha. Raila hawezi kuhujumu ugatuzi ambao ameutetea kwa miaka mingi,” akasema huku akiwaalika wabunge hao kuisoma tena taarifa ya Bw Odinga kuhusu suala hilo kwa makini waielewe.

Kulingana na Bw Etale, kinara huyo wa ODM ni kiongozi wa kitaifa na hawezi kutaka sehemu yoyote ya nchi ibaki nyuma kimaendeleo, haswa ngome yake ya Pwani.

Hata hivyo, aliongeza kuwa Bw Odinga atatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo hivi karibuni.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, aliwaambia viongozi hao, wakiongozwa na Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, kwamba ODM haijawahi na haina mipango ya kubagua Pwani.

“Wale waliolalamika jana (Alhamisi) ni wanachama wa Tangatanga ambao tunajua walitumwa na mkubwa wao kumharibia jina Bw Odinga. Mbona asaliti eneo anakotoka naibu wake Ali Hassan Joho?,” akauliza mbunge huyo, ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa katika ODM.

Mnamo Alhamisi, Bw Baya na wenzake tisa walimkashifu Bw Odinga wakidai aliwasaliti kwa kuwaagiza maseneta wa ODM waunge mkono mfumo ambao utakaopelekea kaunti za Pwani kupoteza fedha nyingi.

Walisema licha ya eneo hilo kuunga mkono chama hicho kwa miaka mingi, kiongozi huyo wa ODM ameendelea kulitenga katika masuala muhimu ya kitaifa.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, walisema kwamba eneo la Pwani litavunja uhusiano na ODM na kusaka washirika wengine wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge wengine wao walikuwa; Mohammed Ali (Nyali), Michael Kingi (Magarini), Aisha Jumwa (Malindi), Sharif Ali (Lamu Mashariki), Andrew Mwadime (Mwatate), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Jones Mlolwa (Voi), Paul Katana (Kaloleni) na Benjamin Tayari (Kinango).

Walitaja hatua ya maseneta kutoka Luo Nyanza; James Orengo (Siaya), Moses Kajwang’ (Homa Bay), Ochilo Ayacko (Migori) na Fred Outa (Kisumu) kuunga mkono mfumo huo kama iliyochochewa na ushauri wa Bw Odinga.

Siku moja kabla ya suala hilo kuwasilishwa rasmi katika seneti ili lijadiliwe na kuamuliwa, Bw Odinga aliwataka maseneta kupitisha mfumo huo unazoziwezesha kaunti 29 zenye idadi kubwa ya watu kupata nyongeza ya fedha huku zingine 19 zikipunguziwa fedha.

Lakini Alhamisi wabunge hao wa Pwani walisema ni usaliti mkubwa kwa Bw Odinga na maseneta kutoka Luo Nyanza kuunga mfumo huo ambao utapelekea kaunti sita za pwani kupoteza takriban Sh6 bilioni.

“Tunawaonya maseneta hao wa Luo Nyanza kwamba hatua yao kuunga mkono mfumo huo italeta talaka ya kisiasa kati yetu na wao.”

“Hata hivyo, wenzangu kutoka maeneo mengine yaliyosalia nyuma kimaendeleo walishirikiana na ndugu na dada zetu wengine na kuangusha hoja hiyo,” akasema Bw Baya.