ODM yalaumiwa kuhusu uongozi wa Joho, Kingi

ODM yalaumiwa kuhusu uongozi wa Joho, Kingi

NA WAANDISHI WETU

WAGOMBEAJI ugavana kupitia Chama cha ODM katika Kaunti za Mombasa na Kilifi, wanajitahidi kujitenga na madai ya uongozi duni ambayo wapinzani wao wanasema yalitokea kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Magavana Hassan Joho na Amason Kingi, walikuwa wamechaguliwa mamlakani kupitia ODM mwaka wa 2013, kisha wakafanikiwa kuhifadhi viti vyao katika uchaguzi wa 2017.

Huku uchaguzi wa Agosti ukizidi kukaribia, wapinzani wa ODM katika kaunti hizo mbili wanazidi kutilia doa uongozi wa kaunti katika vipindi hivyo viwili wakirai wapigakura kutafuta uongozi mpya.

Chama cha ODM kimemsimamisha Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kurithi kiti cha Bw Joho, huku aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, akipeperusha bendera ya chama hicho kwa ugavana Kilifi.

Katika Kaunti ya Mombasa, Chama cha UDA kikiongozwa na aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar, ambaye ndiye mwaniaji ugavana wa chama hicho, hudai kuwa kuchagua mwaniaji wa ODM itakuwa sawa na kuendeleza mfumo wa uongozi ambao umekuwepo tangu mwaka wa 2013.

Wanachama wa UDA katika Kaunti ya Mombasa, humlaumu sana Bw Joho hasa kuhusu madai kwamba familia yake ni miongoni mwa wenye biashara zilizonufaika kwa mfumo mpya wa usafirishaji mizigo kutoka bandari ya Mombasa kwa reli ya SGR hadi Nairobi.

Ufichuzi wa hivi majuzi kwamba kampuni ya familia ya Bw Joho ilipata zabuni kuwa kampuni pekee ya kusimamia mizigo inayoelekea Sudan Kusini kutoka bandarini, umewapa wandani wa Naibu Rais William Ruto, motisha zaidi ya kusukuma ajenda yao dhidi ya viongozi wa ODM.

Katika ziara yake Pwani iliyoanza Ijumaa, Dkt Ruto alijitenga na maamuzi yaliyofanywa na utawala wa Jubilee kuhusu mfumo wa huduma za bandari, akilaumu vinara wakuu wa chama cha kisiasa cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Wale ambao wanafanya wakazi wa Mombasa wazidi kuwa maskini ni wafanyabiashara wa mji huu waliowekeza katika sekta ya bandari. Nikichaguliwa kuwa rais, nitatoa amri kuu ili shughuli zote za bandari zirudishwe Mombasa kwa manufaa ya wakazi na wala si watu binafsi,” akasema.

Katika baadhi ya hotuba zake miezi iliyopita, Bw Joho alitetea biashara za familia yake akisema zabuni wanazopewa na serikali huwa hazipeanwi kwa upendeleo wowote.

Hata hivyo, Bw Nassir amesuka kampeni zake kwa njia ya kushawishi wapigakura kwamba anajisimamia mwenyewe huku akijivumisha kwa kaulimbiu ya ‘mradi wa wananchi’. Wapinzani wake hudai ni ‘mradi wa Joho’.

Katika Kaunti ya Kilifi, ijapokuwa mgombeaji ugavana kwa tikiti ya UDA, Bi Aisha Jumwa, hupiga kampeni dhidi ya uendelezaji wa uongozi wa ODM katika kaunti hiyo, Bw Mung’aro amepata afueni kwa vile Gavana Kingi alihamia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

PAA iliamua kushirikiana na UDA ndani ya Muungano wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Mwili wa mchimba dhahabu wapatikana baada ya miezi 8

Aliyening’inia kwa ndege kushtakiwa leo Jumatatu kwa...

T L