Habari za Kitaifa

ODM yalia kukaziwa fedha zake na serikali

January 19th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

CHAMA cha ODM kimelalamikia “kukaziwa” mgao wa fedha zake na serikali, licha ya Afisi ya Usajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kutangaza kiwango cha pesa ambacho chama hicho kinafaa kupata.

Mnamo Alhamisi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Edwin Sifuna, alisema kuwa kati ya Sh308 milioni ambazo walitengewa na afisi hiyo, wamepokea Sh50 milioni pekee kufikia sasa, hali inayowaathiri sana kifedha.

Bw Sifuna alisema kuwa chama hicho kimekuwa kikikabiliwa na matatizo mengi ya kifedha, hasa kwenye ulipaji wa kodi ya afisi zake na uendeshaji wa shughuli za kuwasajili wanachama wapya.

“Tuko kwenye shughuli za kuwasajili wanachama wetu kote nchini. Hata hivyo, tumelazimika kusimamisha shughuli zetu kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha. Tunairai serikali ya Kenya Kwanza kutoa fedha hizo kwani inaturudisha nyuma kama chama cha kisiasa,” akasema Bw Sifuna, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Bw Sifuna alisema kuwa kwenye makadirio ya kwanza ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa serikali wa 2023/2024, vyama vya kisiasa vilikuwa vitengewe jumla ya Sh6 bilioni, lakini serikali ikapunguza fedha hizo hadi Sh1.6 bilioni.

“Kimsingi, ODM ingepata jumla ya Sh877 milioni, lakini fedha hizo zikapunguzwa hadi Sh308 milioni pekee! Kama hilo halitoshi, serikali bado inatukazia fedha hizo hata baada ya kuzipunguza!” akalalama Bw Sifuna.

Kwenye mgao mpya wa fedha hizo, chama tawala cha UDA ndicho kilipata mgao mkubwa, kwa kutengewa Sh576 milioni.

Hata hivyo, kama ODM, UDA pia imekuwa ikilalamika kwa kutengewa “kiasi kidogo cha pesa”.

Vyama vingine vilivyopata mgao mkubwa ni Jubilee na Wiper, ambavyo vilitengewa Sh135 milioni na Sh72 milioni mtawalia.

Vyama hivyo vinahusishwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Kalonzo Musyoka.