Habari MsetoSiasa

ODM yamcheka Ruto kudai alimpa Raila kazi AU

May 27th, 2019 2 min read

LYDIA NGUGI na RUTH MBULA

VIONGOZI wa Chama cha ODM wamemsuta vikali Naibu Rais William Ruto kutokana na madai yake kwamba alichangia katika uamuzi wa Muungano wa Afrika (AU) kumpa kazi kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga.

Alipokuwa akizungumza Jumapili, Dkt Ruto alidai Jubilee ilitia bidii kuhakikisha AU imempa Bw Odinga kazi ya ubalozi wa miundomsingi Afrika ilhali sasa ameanza kutumia wadhifa huo vibaya.

“Wakati tulipomtafutia kazi AU, kazi yake haikujumuisha biashara ya madini wala dhahabu. Huenda kuna matapeli ambao walimuingiza katika hiyo biashara ya madini na dhahabu ambayo si ya kweli,” alisema.

Lakini jana, Bw Dennis Onyango ambaye ndiye msemaji wa Bw Odinga, na Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed walimkashifu Naibu Rais kwa madai yake ya kuhusika katika kumtafutia kazi Bw Odinga.

Bw Onyango alisema madai ya Bw Ruto ni uongo mtupu kwani hakuhusika kwa njia yoyote kumfanya Bw Odinga kuwa balozi wa masuala ya miundomsingi Afrika katika AU.

“Ruto akipewa fursa anaweza kudai alihusika kwa chochote kile. Tunachofahamu na ninavyoamini ni kwamba Wakenya wanajua Ruto hawezi kushiriki kwa jambo lolote linalomwinua Raila Odinga. Kama alihusika katika mashauriano hayo, basi huenda aliyaingilia ili kuvuruga mipango lakini akashindwa,” akasema Bw Onyango.

Kwa upande wake, Bw Mohammed alisema hakuna vile Naibu Rais anaweza kuaminika kwa chochote anachosema.

Kulingana naye, wiki chache zilizopita Dkt Ruto alisema wazi kwamba Bw Odinga alitaka kukutana naye akakataa, madai ambayo pia yalikuwa yamekanushwa na viongozi wa ODM.

“Unahitaji kuwa na uwezo wa kukumbuka mambo vyema ikiwa unataka kuwa mwongo hodari. Hii siasa ya chuki na matusi ni ngumu,” akasema Bw Mohammed, kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kwingineko, baadhi ya viongozi wa ODM wanamtaka kiongozi wa chama chao pamoja na Rais Uhuru Kenyatta waharakishe shughuli zitakazotoa nafasi kwa kura ya maamuzi.

Wabunge hao walisema muda unayoyoma na inastahili mwongozo kuhusu shughuli hiyo utolewe haraka.

Wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa wa ODM, Bw Opiyo Wandayi, wabunge hao walisema inafaa ieleweke wazi sasa ikiwa kutakuwa na kura ya maamuzi ili shughuli hiyo ijumuishwe kwenye bajeti ya taifa.

“Tusipoandaa shughuli ya kubadilisha Katiba yetu sasa hivi, hatutawahi kufanya hivyo wakati mwingine,” akasema Mbunge huyo wa Ugunja, Kaunti ya Siaya.

Alikuwa ameandamana na wabunge wengine tisa kwenye harambee katika Kanisa la Shirikisho lililoko Suna Magharibi, Kaunti ya Migori mnamo Jumapili ambapo walisema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha umma kuhusu hitaji la marekebisho ya Katiba.

Mbunge wa Ruaraka, Bw Tom Kajwang alisema waliamua kuenda mashinani kuhamasisha umma kuhusu mabadiliko ambayo huenda yakafanywa kwenye Katiba.

Kuhusu ufisadi, viongozi hao walimtaka Rais Kenyatta kuchukua hatua kali dhidi ya maafisa wa serikali wanaofuja mali za umma wakisema mienendo hiyo inayotishia ustawi wa taifa.