Habari MsetoSiasa

ODM yamtaka Dkt Ruto ajiuzulu kwa kumkejeli Rais

August 23rd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimemtaka Naibu Rais William Ruto kujiuzulu kwa kuonekana kumkejeli Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na sakata za uporaji wa fedha za kupambana na janga la Covid-19.

Kwenye kikao na wanahabari Jumamosi katika makao makuu ya chama hicho, Nairobi Mkurugenzi Mkuu wa chama hicho Oduor Ong’wen alisema Dkt Ruto anafaa kumsaidia bosi wake katika vita dhidi ya uovu huo badala ya kujiondolea lawama.

“Kauli ya Naibu Rais Dkt William Ruto kwamba sasa hatalaumiwa kwa wizi wa fedha za Covid-19 ilionyesha kuwa ni sawa kwa fedha kuibiwa kwa sababu hatalaumiwa. Isitoshe, aliashiria kuwa Rais Kenyatta ndio wa kalaumiwa kwa sababu kumtenga. Au aliona wivu kuwa aliachwa nje katika wizi huo,” akasema Bw Ong’wen ambaye alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu Edwin Sifuna.

“Ikiwa Dkt Ruto hataki kumsaidia Rais Kenyatta kupambana na wezi wa fedha za umma, basi hafai kuendelea kushikilia wadhifa wa Naibu Rais. Anafaa kujiuzulu ili Rais atafute mtu mwingine wa kumsaidia kazi,” akasema.

Maafisa hao wawili wa ODM walisema inasikitika kuwa Dkt Ruto amekuwa akitumia muda wake mwingi kuendesha kampeni za kujipigia debe kuhusiana na uchaguzi wa urais 2022 wakati ilhali anapaswa kumsaidia Rais Kenyatta kupambana na maafisa fisadi serikalini.

“Anaendelea kushabikia maovu yanayoendelea serikali kwa imani potovu kwamba kufeli kwa Rais Kenyatta kutaimarisha sifa zake ambazo zimekuwa zikididimia,” akasema Bw Sifuna.

Maafisa hao wawili walisema wataendelea kuhakikisha utendakazi wa serikali, haswa kuhusiana na masuala yanayohusiana na Covid-19, kupitia asasi husika “wala sio kwa kuibua drama na kelele zisizo na maana.”