Habari MsetoSiasa

ODM yapuuzilia mbali juhudi za ‘Punguza Mizigo’

July 25th, 2019 2 min read

LEONARD ONYANGO na OSCAR KAKAI

CHAMA cha ODM kimepinga mswada wa Punguza Mzigo kwa msingi kwamba hauwiani na maono ya mageuzi yanayopigiwa debe na kiongozi wake, Bw Raila Odinga, miongoni mwa sababu nyinginezo.

Kulingana na ODM, mswada huo wa kutaka kufanyia mabadiliko katiba unaofadhiliwa na chama cha Thirdway Alliance chake Ekuru Aukot, ulipuuza muundo wa serikali ambayo itajumuisha jamii zote nchini.

Vilevile, mswada huo haujapendekeza mfumo wa uongozi utakaotoa nafasi ya kuwepo kwa wadhifa wa Waziri Mkuu. Kulingana na Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, mswada wa Punguza Mizigo haujatoa nafasi kwa wadau kuuongezea maoni yao na hivyo basi ukisonga mbele jinsi ulivyo, kuna hofu masuala hayo yataachwa nje.

Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe kupanuliwa kwa serikali itakayojumuisha jamii zote nchini kama njia mojawapo ya kumaliza fujo ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila baada ya uchaguzi.

Chama hicho cha Upinzani pia kinadai kuwa Dkt Aukot aliaandaa mswada huo yeye binafsi bila kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya.

Kulingana na ODM, lengo la mswada wa Punguza Mzigo ni kusambaratisha kamati iliyoundwa na Rais Kenyatta pamoja na kiongozi wa ODM Bw Odinga kukusanya maoni kuhusu namna ya kuunganisha Wakenya, almaarufu kama BBI.

“Mfadhili wa mswada wa Punguza Mzigo Dkt Aukot alikimbilia kukusanya saini kutoka kwa Wakenya kwa lengo la kusambaratisha BBI. Dkt Aukot hata amewahi kwenda kortini kupinga BBI,” akasema Bw Sifuna.

Alipuuzilia mbali msimamo kwamba mswada huo ambao tayari umetumwa katika mabunge ya kaunti zote 47 kujadiliwa na madiwani, utaleta afueni kwa walipa ushuru.

Badala yake, ODM ilidai Punguza Mizigo inalenga kupiga marufuku uteuzi wa wabunge, maseneta na madiwani maalumu, pendekezo ambalo chama cha ODM kinasema litaumiza wanawake.

Chama hicho pia kinasema kuwa pendekezo la kutaka kufutilia mbali maeneobunge 290 utasababisha uhasama wa kikabila haswa katika maeneobunge yaliyo na jamii zaidi ya moja.

Hata hivyo chama hicho kilisema kinakubaliana na Mswada wa Punguza Mzigo kuhusu kupunguzwa kwa idadi ya wabunge lakini hawakubaliani na idadi iliyopendekezwa. Kinakubaliana pia kuwepo urais wa awamu moja yenye miaka saba, mradi tu kuwe na Waziri Mkuu.

Huku hayo yakijiri, jopo la BBI limejitenga na mpango Punguza Mizigo. Wakiwa Pokot Magharibi mnamo Jumatano, Mwenyekiti Yusuf Haji alisema: “Tumekuja kukusanya maoni na hatuelewi lolote kuhusu Punguza Mizigo. Kazi yetu inaeleweka vyema na hatufai kuchanganywa na ile ya Punguza Mizigo. Tumesikia tu kuhusu mpango huo kupitia kwa vyombo vya habari na wanasiasa.”

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa Wakenya kulipa jopo hilo muda limalize kazi yake na kupeana ripoti yake ya mwisho kuhusu mapendekezo ya iwapo katiba itahitaji kufanyiwa marekebisho.

“Sisi hatufanyi siasa bali tunakusanya maoni kuhusu yale Wakenya wanataka,” alisema.

Naibu mwenyekiti, Adams Oloo alisema kuwa wako na kaunti mbili zaidi kabla ya kumalizia kukusanya maoni hayo kote nchini.