Habari MsetoSiasa

ODM yashukuru Rais kuhusu BBI

November 18th, 2019 2 min read

NA JUSTUS OCHIENG’

CHAMA cha ODM kimepongeza Rais Uhuru Kenyatta kutokana na kauli yake kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra wakati wa mkutano kati yake na viongozi wa Mlima Kenya katika ikulu ndogo ya Sagana Ijumaa.

Kupitia taarifa ya Mwenyekiti John Mbadi, chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kimesema matamshi hayo yanaonyesha dhahiri kwamba Rais ana nia njema ya kuunganisha taifa hili.

Bw Mbadi alisifu mtazamo wa Rais kuhusu uchaguzi mdogo wa Kibra, akisema kauli yake inaoana na ile ya ODM kuhusu kura hiyo.

“Kwa niaba ya chama cha ODM na Wakenya wote ambao wamemakinika kuona taifa lenye umoja na amani, ningependa kumshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kusimama na ‘handisheki’ na BBI ambazo ni njia muhimu ya kuwaunganisha Wakenya,” ikasema taarifa ya Bw Mbadi.

“Pia tungependa kumshukuru Rais Kenyatta kwa kauli yake kwamba uchaguzi mdogo wa Kibra ulikuwa amani, ishara tosha kwamba kupitia umoja wa viongozi wetu, uchaguzi wa amani unaweza kufanyika siyo tu Kibra pekee bali eneo lolote nchini,” ikaongeza taarifa.

Taarifa ya ODM inajiri huku cheche za maneno zikiendelea kuhusu uchaguzi mdogo wa Kibra, Naibu Rais Dkt William Ruto na wabunge wa Tangatanga wakilalamikia ghasia na vitisho dhidi ya wabunge wa Jubilee wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi.

Ni kutokana na ghasia hizo ambapo Dkt Ruto alimtaka Bw Odinga kuomba radhi hadharani huku ODM ikishikilia kwamba wabunge wa Jubilee walikumbana na ghadhabu za wapigakura waliotibua njama yao ya kununua kura kabla na wakati wa uchaguzi huo.

Rais Kenyatta pia akihutubu katika ikulu ya Sagana aliwashukuru wapigakura wa Kibra kwa kufanya uchaguzi wa amani, matamshi yaliyokinzana na aliyoyatoa Dkt Ruto ambaye amekuwa akivamia Bw Odinga kuhusu Kibra kupitia mtandao wa kijamii.

Kwenye taarifa yake, Bw Mbadi pia aliwashukuru Wanakibra kwa kutekeleza majukumu muhimu kuhakikisha uchaguzi huo ulikuwa wa amani.

“Kutokana na uchaguzi huo, wakazi wa Kibra waliandikisha historia kwa kuongoza katika kuzaliwa upya kwa taifa letu,” akasema Bw Mbadi.

Aidha mbunge huyo wa Suba Kusini aliwaomba Wakenya na wafuasi wa ODM waunge mkono ripoti ya BBI ambayo inatarajiwa kukabidhiwa Rais na Bw Odinga hivi karibuni.

Ingawa hivyo, alisisitiza kauli ya Rais na Bw Odinga kwamba BBI haihusiani kivyovyote na siasa za 2022 au azma ya Urais ya mtu binafsi.

Vilevile alitoa wito kwa viongozi hao wawili wakuu kutopoteza dira kuhusu nia yao ya kuleta taifa hili pamoja huku akiwaahidi uungwaji mkono wa viongozi wote waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM.