ODM yashutumiwa kwa kupendekeza kung’olewa mamlakani kwa Chebukati

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa kisiasa kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa wameshutumu wenzao wa ODM kwa kupendekeza kuondolewa afisini kwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wanasiasa hao wanaogemea mirengo ya vyama vya Amani National Congress (ANC) na United Democratic Alliance (UDA) walidai wito huo wa ODM unachangiwa na “dalili kwamba anayetarajiwa kuwa ndiye atakuwa mgombeaji wao, Raila Odinga, atabwagwa katika kinyang’anyiro cha urais”.

Wakiongea Jumamosi katika hafla ya mazishi katika Kaunti ya Kakamega, Seneta Cleophas Malala, Mbunge wa Lugari Ayub Savula na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale waliapa kuzuia juhudi zozote za kumng’atua Bw Chebukati.

“Hatutakubali Raila kumfuta kazi Bw Chebukati kwa manufaa yake ya kibinafsi. Tunamtaka mwenyekiti huyo na makamishna wenzake kuendelea kuchapa kazi bila woga wowote,” akasema seneta Malala.

“Hatuwezi kuvumilia mienendi hii ya kubadilishwa kwa makamishna wa IEBC kila uchaguzi unapokaribia. Raila na watu wake hawafai kujifanya kana kwamba wao ndio wanamiliki Kenya. Kenya ni yetu sote,” akafoka Dkt Khalwale.

Kwa upande wake Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale alishutumu wabunge wa ODM wanaoshinikiza kuondolewa kwa Bw Chebukati akisema hamna sababu maalum ya kuondolewa kwake mamlakani.

“Lazima kuwe na sababu maalum ya kuondolewa mamlakani kwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati na makamishna wenzake. Kufikia sasa watatu hao wamekuwa wakifanya kazi nzuri licha ya kuwepo kwa pengo katika nafasi za makamishna wanne waliojiuzulu mnamo 2018,” akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake rasmi ya mtandao wa Twitter.

“Inasikitika kuwa kila mwaka uchaguzi unapokaribia, kutokana na woga au sababu nyinginezo, wanasiasa huanzisha wimbo wa kumwondoa mwenyekiti wa IEBC na makamishna wenzake. Hatutakubali hali kama hiyo kutokea nchini wakati huu tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu,” akaongeza Bw Duale ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto.

Huku akinukuu ripoti ya tume ya kuchunguza chanzo cha ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu nchini Afrika Kusini Johanns Kriegler, Bw Duale alisema mabadiliko katika IEBC hayafai kutekelezwa mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

“Viongozi hawa walikuwa wapi miaka minne iliyopita wakati Chebukati na wenzake walikuwa wakihudumu? Je, mbona ni wakati huu ambapo wamegundua kuwa Chebukati na wenzake hawafai kushikilia nyadhifa hizo?” akauliza mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Mnamo Ijumaa, wanasiasa wa ODM wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Homa Bay Gladys Wanga, walianzisha wito wa kuong’olewa kwa Bw Chebukati wakisema chama hicho hakina imani naye.

Walisema hii ni kufuatia kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017.

“Sioni ikiwa mimi Gladys Wanga nitakubali kushiriki uchaguzi mkuu ujao chini ya usimamizi wa Chebukati. Sina imani naye hata!” akasema Bi Wanga wakati wa mazishi ya babake Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang, Mzee David Ajwang Nyakwamba.

Marehemu pia ni babake Mbunge wa Ruaraka T J Kajwang’ na aliyekuwa Seneta wa Homa Bay marehemu Otieno Kajwang’ almaarufu “Mapambano”.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi alimshauri mwenyekiti huyo wa IEBC kusitisha utekelezaji wa Mpango wa Maandalizi ya Uchaguzi (EOP) kwa wiki tatu ili kusubiri uteuzi rasma wa makamishna wanne wapya walipendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“IEBC isimamisha shughuli zote za maandalizi kama vile ununuzi wa vifaa vya uchaguzi kama vil mitambo ya kieletroniki na uagizajiwa karatasi za kupigia kura kwa majuma matatu hivi hadi makamishna wapya waingie afisini,” akasema Bw Wandayi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masuala ya kisiasa katika ODM.

Kauli yake iliungwa mkono na Seneta wa Kisumu Fred Outa ambaye pia alihudhuria mazishi hayo.

Kioongozi wa ODM Raila Odinga ambaye alihudhuria hafla hiyo alikwepa kuzungumzia suala hilo na badala yake akasema amepata mbinu mpya za kupenyeza katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Mnamo Agosti 5, 2021, Rais Kenyatta alipendekeza Francis Wanderi, Justus Abonyo, Juliana Cherera na Irene Cherop kuteuliwa kuwa makamisha wapya wa IEBC. Ikiwa wataidhinishwa na Bunge, wanne hawa watajaza nafasi za Dkt Roselyne Akombe, Consolata Nkatha Bocha, Mary Mwanjala na Dkt Paul Kurgat waliojiuzulu mnamo Aprili 18, 2018 kutoka na sababu mbalimbali.