Habari MsetoSiasa

ODM yasukuma Uhuru awapige kalamu mawaziri ‘fisadi’

April 2nd, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kimemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwafuta kazi mawaziri wanaochunguzwa kwa madai ya ufisadi atakapohutubia Bunge kesho.

Kulingana na chama hicho, hatua hiyo itadhihirisha kujitolea kwake kupambana na ufisadi.

“Namwambia Uhuru Kenyatta, ukianza kulegea unapoona vita vya ufisadi vimekaribia mawaziri au karibu na Ruto, hatutafanikiwa kushinda,” akasema Kinara wa Wachache katika Seneti, James Orengo.

Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi aliunga mkono kauli hiyo akisisitiza kuna njia nyingi za kupambana na ufisadi kuliko kuwakamata na kuwashtaki pekee.

Kulingana naye, inafaa Rais atumie mamlaka yake ipasavyo bila uwoga.

“Kuondoa mawaziri ni jambo rahisi sana kwa sababu Rais mwenyewe anaweza kuamka tu akaagiza waondoke. Inafaa Rais awaagize kujiondoa mamlakani hadi uchunguzi dhidi yao ukamilike,” akasema Bw Mbadi.

Awali wikendi, Mbunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Bw Oburu Oginga alidai Bw Odinga atajiondoa kwenye mwafaka wake na Rais Kenyatta endapo Rais hatadhihirisha kujitolea kuadhibu maafisa wakuu serikalini waliohusishwa na ufisadi.

“Kakangu Raila amejitahidi kwenye vita dhidi ya ufisadi kwa sababu Rais Uhuru amejitolea. Lakini kama Rais atakubali kuchanganywa akili na washukiwa hadi alegeze msimamo wake, Raila ataondoka tu kwenye handsheki,” akanukuliwa Bw Oburu.

Bw Orengo alitoa wito kwa Rais Kenyatta kuhimiza wabunge watumie mamlaka yao kutimua mawaziri waliotajwa kwenye sakata za ufisadi atakapohutubu kesho.

Kufikia sasa, mawaziri kadhaa wakiwemo Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Henry Rotich (Fedha), Simon Chelugui (Maji) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi), wamekuwa wakihojiwa na maafisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuhusu ufujaji wa mabilioni ya fedha za umma, huku ikiaminika kuna mawaziri watatu ambao huenda wakashtakiwa.

“Kwa vile sitakuwa bungeni Alhamisi, ninamtaka Rais awahimize wabunge kuwatimua mawaziri wafisadi. Vita dhidi ya ufisadi si jukumu la polisi na EACC pekee. Bunge linaweza kutumiwa kukabiliana na ufisadi. Bunge linaweza kumsaidia Uhuru asimamishe kazi mawaziri waliotajwa,” akasema Seneta huyo wa Kaunti ya Siaya.

Alikuwa akizungumza Jumatatu jioni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika eneobunge la Ugenya, ambapo mgombeaji wa ODM ni Bw Chris Karan. Ushindi wake wa 2017 ulifutiliwa mbali na mahakama baada ya malalamishi kuwasilishwa na aliyekuwa mbunge, Bw David Ochieng.

Katiba inamhitaji Rais kuhutubia Bunge angalau mara moja kila mwaka ili kutoa ripoti kuhusu hatua zilizopigwa na serikali yake katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuhusu uadilifu na usalama wa kitaifa.

Mnamo 2015, Rais Kenyatta alishangaza wengi alipotumia hotuba hiyo kuwasilisha orodha ya maafisa wakuu serikalini waliodaiwa kuhusika katika ufisadi, wakiwemo mawaziri.