Habari MsetoSiasa

ODM yatarajia BBI kutia nguvu 'risasi' ya Raila

June 6th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Siaya James Orengo ameelezea matumaini kuwa refarenda ijayo itaiwezesha ODM kufikia lengo lake kutwaa mamlaka ili kuchangia katika uboreshaji wa uongozi wa taifa hili.

Ijapokuwa kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga hajatangaza wazi kama atawania urais katika uchaguzi ujao, wafuasi wake wengi wanatarajia atakuwa katika debe.

Katika chaguzi zilizopita za urais, Bw Odinga alishinikiza mabadiliko makubwa katika sheria za uongozi na uchaguzi wa kisiasa na wadadisi wanaona historia inajirudia katika shinikizo lake la sasa ambalo limepata uungwaji mkono kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Azma kuu ya chama chochote cha kisiasa ni kutwaa mamlaka. Lakini sisi kama ODM chini ya uongozi wa kinara wetu Raila Odinga tunapania kufikia hili chini ya mchakato wa BBI na handisheki ambayo nguzo zake zitatekelezwa kupitia mageuzi yajayo ya katiba kupitia kura ya maamuzi,” akaeleza Bw Orengo.

Bw Orengo alisema mabadiliko ya uongozi yanayotekelezwa katika Seneti na Bunge la Kitaifa sasa ni sehemu ya maandalizi ya kura ya maamuzi kwani asasi hiyo ni kiungo muhimu katika ufanikishaji wa ajenda hiyo.

“Na jana sisi kama viongozi wa Seneti kupitia Spika wetu Kenneth Lusaka tulitangaza waziwazi kwamba tutafanikisha ajenda ya mageuzi ya katiba alivyopendekeza Rais Uhuru Kenyatta alipoongoza sherehe za Madaraka Dei,” akaongeza Seneta huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga.

Mnamo Alhamisi uongozi wa Seneti ulifanya mkutano katika mkahawa mmoja eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos, ambapo viongozi wa mirengo yote waliafikiana kuunga mageuzi ya katiba.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni kiongozi wa wengi Samuel Poghisio, naibu wake Fatuma Dullo, Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata, mwenzake wa upande wa wachache Mutula Kilonzo Junior miongoni mwa wengine.

Naye kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohammed akasema; “Unajua wazi kwamba Baba (Bw Odinga) ni mmoja wa waasisi wa BBI inayopendekeza kura ya maamuzi. Bila shaka atakuwa mhusika mkuu katika faida itakayotokana na mchakato huo na ambayo vile vile itafurahiwa na taifa zima.”

Bw Mohammed ambaye ni mbunge wa Suna Mashariki na mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM alishikilia kuwa kura ya maamuzi kufanikisha mageuzi ya katiba ifanyike kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Na si ulisikia juzi Baba akisema shughuli hiyo inaweza hata kufanyika mwaka huu. Si mnaona tunatengeneza barabara kwa kuondoa visiki katika seneti na bunge la kitaifa?” akaongeza.

Alikuwa akirejelea mchakato unaoendelea wa kuwaadhibu maseneta na wabunge ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto na wanaopinga muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.