Habari MsetoSiasa

ODM yatema 9 Kibra huku Jubilee na ANC zikijitosa kwa kinyang'anyiro

August 28th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimewafungia nje tisa miongoni mwa watu waliojitokeza kutaka kuwania kiti cha ubunge cha Kibra kwa tiketi yake katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 7.

Hayo yalijiri huku vyama vya Jubilee na ANC vikijitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano wa ODM, Philip Etale, chama hicho kiliwasilisha majina ya watu 11 pekee kati ya 20 waliokuwa wakisaka tiketi yake ili kuwania kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha Ken Okoth mwezi uliopita.

“Wagombeaji wengine waliachwa nje baada ya kukosa kutimiza sheria za chama na masharti mengine ya uteuzi,” akasema Bw Etale.

“Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi imetuma ujumbe kuhusu uamuzi huo na ikawasilisha orodha ya wagombeaji 11 ambao wametimiza sheria na masharti yaliyowekwa na ODM,” akaongeza.

Kufikia Jumanne adhuhuri, wagombeaji ambao walikuwa wameidhinishwa kushiriki mchujo wa ODM ni Awino Christine Odhiambo, Orero Peter Ochieng, Sine Tony Ogola Sira, Ojijo Reuben William Ayako, Oguwa Stephen Okello na Okoth Benard Otieno.

Wengine ni Obayi Obaricks Eric Ochieng’, Owino Brian Shem, Millar John Otieno, Musungu Benson na Owade Lumumba Patrick.

Hao ndio watashiriki katika kura ya mchujo ambayo itafanyika Jumamosi hii katika vituo vyote vya upigiaji kura vinavyotambuliwa na IEBC katika eneo bunge la Kibra.

“Zoezi hilo litafanywa kwa njia ya upigaji kura wa moja kwa moja na chama kimejitolea kuhakikisha kuwa litaendeshwa kwa njia huru na haki. Ni wanachama wa ODM pekee watakaoruhusiwa kushiriki katika zoezi hilo,’ akasema Bw Etale.

Chama cha Amani Natinal Congress (ANC) nacho jana kilimtangaza rasmi aliyekuwa msadizi wa Bw Odinga, Eliud Owalo kuwa mgombeaji wake Kibra.

Bw Owalo, ambaye alihama ODM mapema mwezi huu, alizunduliwa katika sherehe iliyoongozwa na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi.

Nacho chama cha Jubilee kiliwataka wale wanaotaka kuwania kiti cha Kibra kwa tiketi ya chama hicho kutuma maombi kufikia kesho jioni.