Habari Mseto

ODM yatema wagombeaji tisa katika mchujo wa Kibra

August 28th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimewafungia nje tisa miongoni mwa watu waliojitokeza kutaka kuwania kiti cha ubunge eneobunge la Kibra kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 7, 2019.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa mawasiliano ODM Philip Etale, chama hicho kiliwasilisha majina ya watu 11 pekee kati ya 20 waliokuwa wakikimezea mate kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha Ken Okoth Julai 26, 2019.

“Wagombeaji hao tisa waliachwa nje baada ya kukosa kutimiza sheria za chama na masharti mengine ya uteuzi,” akasema Bw Etale.

Akaongeza: “Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi imetuma ujumbe kuhusu maamuzi hayo na ikawasilisha orodha ya wagombeaji ambao wametimiza sheria na masharti yaliyowekwa na ODM.”

Kufikia Jumanne adhuhuri, wagombeaji ambao walikuwa wameidhinishwa kushiriki mchujo baada ya kutimiza sheria na masharti husika ni wafuatao; Awino Christine Odhiambo, Orero Peter Ochieng, Sine Tony Ogola Sira, Ojijo Reuben, William Ayako, Oguwa Stephen Okello na Okoth Benard Otieno.

Wengine ni; Obayi Obaricks Eric Ochieng’, Owino Brian Shem, Millar John Otieno, Musungu Benson na Owade Lumumba Patrick.

Wagombeaji hawa ndio watashiriki katika kura ya mchujo ambayo itafanyika Jumamosi Agosti 31, 2019 katika vituo vyote vya upigiaji kura vinavyotambiliwa na IEBC katika eneobunge la Kibra.

“Shughuli hiyo itafanyiwa kwa njia ya upigaji kura wa moja kwa moja na chama kimejitolea kuhakikisha kuwa inaendeshwa kwa njia huru na haki. Na ni wanachama wa ODM pekee wataruhusiwa kushiriki katika shughuli hiyo,” akasema Bw Etale.