ODM yatoa onyo kwa wabunge wake kuhusu BBI

ODM yatoa onyo kwa wabunge wake kuhusu BBI

GEORGE ODIWUOR na KNA

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM), kimepinga mipango ya kundi la wabunge ya kutaka kufanyia marekebisho baadhi ya vipengee kwenye katiba kupitia bunge, kikisema kwamba, viongozi wake katika bunge la taifa na seneti hawakushirikishwa kwenye mipango hiyo.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, John Mbadi alisema kwamba, ameagiza wanachama kutoshiriki katika juhudi za kubadilisha katiba kupitia bunge zinazoendelezwa na baadhi ya Wabunge.

Bw Mbadi ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa pia alisema kwamba, wabunge wa vyama vingine vya upinzani wameagizwa kutounga mpango huo.

Kundi la wabunge 13 limetambua mapendekezo kumi yasiyozozaniwa katika Mswada wa Kubadilisha Katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI) wanayotaka yapitishwe kupitia bunge.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu kuzima mchakato wa kubadilisha katiba kupitia kwa BBI ikisema haukuwa wa kikatiba.

Miongoni mwa masuala ambayo wabunge hao wanataka yajadiliwe ni kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake wawili, kanuni ya uwakilishi wa jinsia, sheria za usalama, kaunti kutengewa pesa zaidi, mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na kubuniwa kwa maeneobunge mapya.

Lakini ODM inapinga hatua hiyo ikisema kwamba, chama hicho hakijaamua kutumia bunge kubadilisha katiba ingawa baadhi ya wanachama wake, akiwemo seneta wa Homa Bay Moses Kajwang na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo wameonyesha nia ya kuunga hatua hiyo.

Bw Mbadi aliongea na wanahabari mjini Homa Bay ambapo alisema ana imani Mahakama ya Rufaa itabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliosimamisha mchakato wa BBI.

Aliwahimiza Wakenya kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ambao utatoa mwelekeo kuhusu ni lini kura ya maamuzi itafanyika.

Lakini mbunge wa Garissa mjini Aden Duale, alivitaka vyama vya kisiasa nchini kuungana kuokoa Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kupitia bunge. Akizungumza katika hafla ya kuchangisha pesa mjini Garissa, Duale alisema hakuna wakati wa kutosha wa kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na pengine uamuzi wa rufaa nyingine katika Mahakama ya Juu kuwezesha kura ya maamuzi kuandaliwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Hatuna shida na BBI ikiwa hatutapoteza maeneobunge ya Ijaara na Wajir Kusini. Ninataka kuomba vyama vya kisiasa kuungana kwa sababu katiba inaruhusu kufanyiwa marekebisho kupitia bunge, wabunge wapitishe vipengele visivyohitaji kura ya maamuzi tukisubiri uamuzi wa korti,” alisema,” Duale.

Duale alikuwa miongoni mwa wabunge 83 waliopiga kura ya kukataa mswada wa BBI bungeni mapema mwezi uliopita.

Wanaounga mpango wa bunge kubadilisha katiba wanasema utakuwa ushindi kwa Wakenya wote hasa baada ya Spika Justin Muturi kuunga juhudi zao.

You can share this post!

Madaraka Dei bila uhuru

Mauaji: Wapenzi wa kando washukiwa