Habari

ODM yavitaka vyama tanzu vya NASA vikomeshe siasa za 2022

February 28th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

KATIBU Mkuu wa Chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna, amepuuzilia mbali vyama tanzu vya Muungano wa NASA vinavyotaka upinzani uanze kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika kikao chake cha kwanza cha wanahabari Jumatano tangu achaguliwe kwenye wadhifa huo wiki iliyopita, Bw Sifuna alisema lengo kuu la ODM ni kupigania haki ya chaguzi zilizofanywa mwaka uliopita kabla mjadala wowote kuhusu 2022 uanze.

“Tunataka kila mmoja alenge macho yake kwa adui halisi wa wananchi ambayo ni utawala wa kiimla wa Jubilee. Wale wanaotaka kutuzuia tunawaambia kama nyinyi ni waoga wa kukabiliana na utawala wa kiimla msituzuilie njiani, mturuhsu tuendeleza kazi hiyo,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika makao makuu ya chama hicho Nairobi ambapo aliandamana na manaibu wake ambao ni aliyekuwa seneta maalumu Dkt Agnes Zani na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Busia, Bi Florence Mutua.

Viongozi kadhaa wa vyama vya Wiper na Amani National Congress wamekuwa wakiambia viongozi wao, Bw Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi mtawalia, wasahau kuhusu uchaguzi uliopita na waanze kujiandaa kwa uchaguzi ujao.