ODM yawataka wanaolenga tiketi Kibra wajiepushe na vurugu

ODM yawataka wanaolenga tiketi Kibra wajiepushe na vurugu

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimewaonya wagombea wake wote kwamba wale watakaothubutu kusababisha vurugu katika kura ya mchujo itakayofanyika Jumamosi Kibra, watakamatwa na kufurushwa kutoka chama hicho.

Na Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) Judith Pareno mnamo Jumanne aliwahakikishia wagombea wote kwamba shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia huru, haki na yenye uwazi huku akisema maandalizi yote yamekamilika.

“Tumejiandaa barabara. Tumekodisha vituo vyote ambavyo vitatumika kwa kura hiyo ya mchujo na wagombea wote wamepewa hakikisho kwamba shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia huru na haki,” akasema Bi Pareno.

“Kwa hivyo, wagombea ambao watajaribu kuvuruga shughuli hiyo watakamatwa na polisi na chama hakitasita kuwafukuza kabisa,” akaonya.

Jumla ya wagombea 11 watang’ang’ania tiketi ya ODM ili atakayefanikiwa aipeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 7, 2019.

Wao ni pamoja na; Awino Christone Odhiambo, Orero Peter Ochieng’, Sine Tony Ogola Sira, Ojijo William Reuben Ayacko, na Oguwa Stephen Okello.

Wengine ni; Okoth Bernard Otieno, Obayi Obaricks Erick Ochieng’, Owino Brian Shem, Millar John Otieno, Musungu Benson na Owade Lumumba Patrick.

Majina ya maajenti

Bi Pareno, ambaye ni Seneta Maalum alisema kuwa wagombea wote walikuwa wametarajiwa kuwasilisha majina ya maajenti wao katika makao makuu ya ODM kufikia Jumanne jioni.

“Maajenti hao watapewa ushauri kuhusu namna ya kusimamia shughuli huku wakionywa kujiepusha na virugu ambazo zitawaweka pabaya wagombeaji watakaowasilisha,” akasema.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ameambia Taifa Leo kwamba afisi kuu imetoa usaidizi wote ambao bodi ya uchaguzi iliitisha ili iweze kuendesha mchujo huo kwa njia itakayoridhisha wagombea wote.

“Tumesikiza maoni ya wanachama wote wa chama chetu katika eneo la Kibra na walisema wanapendelea uteuzi ambapo wanaruhusiwa kupiga kura moja kwa moja. NEB iliandaa bajeti na ikatuwasilishia ambayo tulipitisha bila marekebisho yoyote kwa sababu hatukutaka visingizio kutoka kwa bodi hii baadaye,” Bw Sifuna akasema.

“Kura ya mchujo ni sawa na uchaguzi na ndio maana sisi kama afisi kuu tunauchukulia kwa uzito zaidi mchakato huu,” akaongeza.

Bw Sifuna alisema ODM imeomba huduma za ulinzi kutoka kwa Kamanda wa Polisi katika kaunti ya Nairobi kwa sababu “usalama huwa ni changamoto kuu katika shughuli kama hiyo”.

“Kwa kulingana nasi katika afisi kuu tumeipa bodi kila kitu ambacho walihitaji. Na NEB imekuwa ikishauriana nasi nyakati zote katika maandalizi yao,” akaeleza.

Bw Sifuna pia alikariri kuwa ODM imewapa polisi ruhusa ya kuwakamatwa mtu yeyote ambaye atathubutu kuvuruga zoezi hilo.

“Wakati huu hatuchezi. Yeyote atakayechochea fujo atakamatwa na kufungwa jela. Kisha tutamfukuza kutoka chama cha ODM kwa sababu hatutavumilia ghasia,” akasema.

Atakayeibuka mshindi Jumamosi inatarajiwa atapambana na McDonald Mariga wa Jubilee, Eliud Owalo wa ANC, Dorn Anaclet wa DP na Butichi Khamisi wa Ford Kenya.

Hata hivyo yapo malalamishi kwamba Mariga alitangazwa mgombea wa Jubilee kwa utaratibu uliokiuka demokrasia chamani.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge Ken Okoth.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Kimbelembele, si kiherere huonyesha...

Nauli yapanda shule zikifunguliwa

adminleo