Makala

ODONGO: Kaunti zipunguze ubadhirifu, ziwekeze kwa miradi inayofaa

April 2nd, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

UBADHIRIFU wa fedha za umma umeendelea kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa ugatuzi, kaunti ya Kisumu ikigonga vichwa vya habari wiki jana kwa kumnunua ng’ombe wa maziwa kwa Sh3.7 milioni 2018.

Kulingana na ripoti hiyo ya mwaka wa kifedha 2017/18, serikali ya Gavana Anyang’ Nyong’o, ilikuwa imetenga fedha hizo kununua ng’ombe 27 ilhali ni mmoja pekee aliyewasilishwa huku stakabadhi nyingine za kuthibitisha iwapo wengine walinunuliwa zikikosekana.

Serikali ya kaunti ilikusudia kuwapa wakulima kutoka maeneobunge yote saba ya Muhoroni, Nyando, Seme, Nyakach, Kisumu ya Kati, Kisumu Magharibi na Kisumu Mashariki ng’ombe hao kama njia ya kuendeleza kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Kwanza kabisa kama mzaliwa wa kaunti hiyo, ufanisi wa mradi wa kilimo cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni jambo gumu kufanikiwa. Kisumu huwa na kiwango cha juu cha joto na kilimo hicho hushamiri sana katika maeneo yenye baridi.

Eneo la Nyando ambako baadhi ya ng’ombe hao wangepelekwa, limetengwa kwa miaka na mikaka, halina miundo msingi bora na hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara wakati wa mvua, na jua kali wakati wa kiangazi.

Eneo hili pia lina mbu wengi hatari kwa mifugo kutokana na kilimo cha mpunga kinachoendelezwa na pia kuwa karibu ba Ziwa Viktoria.

Badala ya ng’ombe hao, kaunti ingetafuta mbinu ya kuinua maisha ya wakulima wengi wanaotegemea kilimo hicho cha mpunga katika eneo Tambarare la Kano.

Sehemu kubwa ya Kisumu Mashariki, Kati na Magharibi inakaliwa na makazi, mitaa na jiji la Kisumu nayo Seme ikitawaliwa na ukame kila mara.

Kilimo cha miwa kinatawala sehemu kubwa ya Muhoroni huku Nyakach ikikumbwa na wizi wa mara kwa mara wa mifugo jamii jirani kutoka kaunti ya Kericho, hali inayowahofisha wananchi kushiriki ufugaji wa ng’ombe hata wale wa kawaida.

Inaonekana mradi huu ulilenga kunufaisha viongozi wachache wa kaunti kwasababu kuna uwezekano finyu kwamba ungefaulu na viongozi wa sasa wanafahamu hilo.

Ni kutokana na ufisadi huu ambapo asasi kama EACC na asasi nyingine zinafaa kuchukua hatua kali na kuwanasa wanaohusika na miradi isiyofaa kaunti ili kujiongezea utajiri.

Kuna miradi mingi katika kaunti ya Kisumu ambayo inaweza kufaulu na kuinua maisha ya wananchi kuliko hii inayoanzishwa na baadaye kutumika na wanasiasa kuifilisi kaunti kifedha.

Kati yao ni kuwekeza katika kilimo cha miwa, mpunga, mtama na kuyainua maisha ya wavuvi wa samaki Ziwa Viktoria na hata kumaliza gugumaji ziwani humo.