Maoni

ODONGO: Kazi ya AU ikae iwapo nia ni kumfunga Raila mdomo

May 7th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

UTAWALA wa Kenya Kwanza unastahili kufahamu kuwa azma ya kupata kazi ya Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) haiwezi kumshika mateka Kinara wa Upinzani Raila Odinga na kumzuia kukosoa serikali.

Wikendi baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza waliingiwa na joto baada ya Bw Odinga kuishambulia vikali serikali kuhusu maovu yanayoendelea na uongozi mbaya nchini.

Akiwa katika mtaa wa Mathare, Nairobi alikopeleka chakula cha msaada kwa wahanga wa mafuriko, Bw Odinga aliwashambulia baadhi ya mawaziri katika utawala wa sasa aliosema ni watu wasiofahamu chochote kuhusu masuala ya uongozi serikalini.

Alitoa mfano wa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ambaye alisema utendakazi wake hauwezi kulinganishwa na ule wa marehemu Profesa George Magoha ambaye alisimamia wizara hiyo kwa ustadi mno.

Pia alishutumu utawala wa sasa aliosema baadhi ya wanaoutumikia ni wale ambao wanajali tu matumbo yao na wamebobea katika ufisadi. Pia alimtaka Rais Ruto atangaze mafuriko kama janga la kitaifa ili Wakenya walioathiriwa wapate misaada ya kujikwamua.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza walimjibu Bw Odinga na kushangaa kwa nini kiongozi huyo wa ODM amejitokeza tena kushambulia serikali ambayo inampigia upatu apate kazi ya AUC.

Mwanzo ni vyema serikali hii ifahamu kuwa wengi wa Wakenya hawajafurahishwa na hatua ya Bw Odinga kusaka kazi AUC. Hii ni kwa sababu ndiye kiongozi pekee ambaye sauti yake inasikika nchini akiwatetea wanyonge.

Wakati ambapo Raila alitangaza kuwa anaendea kazi ya AUC, Wakenya wengi wakiwemo wale waliopigia kura serikali hii waliingiwa na jakamoyo, wakitilia shaka azma yake na kumtaka asalie Kenya kuwatetea.

Ni kweli Raila amekuwa sura ya upinzani na amekuwa akishindwa katika njia tatanishi katika chaguzi tangu 2007.

Bado ana azma ya kuwania kiti cha urais mnamo 2027 na hilo huenda linahofisha viongozi wa sasa serikalini.

Iwapo serikali inapigia upato Raila aelekee AUC ndipo ikose mkosoaji, basi imenoa kwa sababu jinsi mbunge huyo wa zamani amekuwa akiendesha siasa zake, itakuwa vigumu sana kwake kunyamazia maovu ambayo Wakenya wanatendewa.

Suala la AUC si kifo na hata iwapo Raila atakosa nafasi hiyo bado ana haki ya kuja kuwania urais nchini mnamo 2027. Kuna baadhi ya viongozi ambao hata waliwahi kupata hicho cheo cha AUC kisha wakakiacha na kuwania Urais kama Dlamini Zuma mnamo 2017 katika taifa lake la Afrika Kusini.

Pili, viongozi wa Kenya Kwanza wanastahili wakubali kukosolewa badala ya kulalamika. Kukosolewa kwao kunastahili kuwarekebisha ili wahudumie Wakenya vyema wala hawafai kufasiri kila kauli ya Raila kuwa ni siasa.

Kujaribu kutumia suala la AUC kumpiga vita Raila hakutawasaidia kitu. Serikali inaweza kupendekeza jina la Raila kwa AUC na bado akose kura ya Rais Ruto kwa sababu kura hiyo huwa ni siri.

Matamshi ya viongozi hao katu hayatatetemesha Raila na kile serikali inafaa ifanye ni kuwawajibikia Wakenya na kuwakwamua kutokana na majanga ya sasa na pia kuimarisha uchumi wa nchi.