ODONGO: Kitui, Kibwana, Muturi na Karua wana mtihani

ODONGO: Kitui, Kibwana, Muturi na Karua wana mtihani

Na CECIL ODONGO

MUUNGANO wa kisiasa kati ya Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana, Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Waziri wa zamani Dkt Mukhisa Kituyi hauwezi kutikisa mawimbi ya kisiasa hapa nchini.

Wanasiasa hao wanne badala yake wanatumia kuungana kwao katika kusukuma nafasi yao ya kujumuishwa katika mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga ambao wanaonekana kuwa kifua mbele katika mbio za kuingia ikulu mnamo 2022.

Mwanzo, wanasiasa hao wanne hawana ushawishi wowote wa maana katika maeneo wanakotoka na hata kwingine nchini kama Dkt Ruto na Bw Odinga.

Badala yake wanatazamwa kama wasomi wa sheria ambao wanafaa sana wajihusishe na masuala ya kortini au kwenye kumbi mbalimbali wakiwafunza wanavyuo.

Kwa mtazamo wa wengi, Bi Karua, Profesa Kibwana na Dkt Mukhisa Kituyi wanaunganishwa tu na matukio ya zamani ya kupigania mfumo wa vyama vingi nchini miaka ya 80 na mapema miaka ya 90.

Kama tu Bw Odinga ambaye alikuwa mfungwa wa kisiasa enzi hizo, watatu hawa pia walipitia dhuluma dhidi ya utawala wa chama cha Kanu, mara nyingi wakiongoza maandamano ya kupigania mageuzi dhidi ya serikali ya aliyekuwa Rais wa wakati huo marehemu Daniel Toroitich Arap Moi.

Hata hivyo, kizazi cha sasa ambacho wapigakura wake wengi ni vijana, hawana haja na historia hiyo kwa kuwa baadhi yao hata hawakuwa wamezaliwa enzi hizo.

Kwa hivyo, kutumia kigezo cha kupigania demokrasia nchini hakuwezi kuwavunia kura zozote za maana hasa miongoni mwa vijana.

Ingawa Profesa Kibwana, Dkt Kituyi na Bw Muturi wametangaza kuwa watawania Urais, uwezekano wa mmoja wao kufaulu kuongoza Wakenya ni finyu.

Profesa Kibwana alihudumu kama mshauri wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki kuhusu masuala ya kisheria.

Pia amehudumu kama Gavana wa Makueni kwa mihula miwili; nafasi ambayo kwa kweli ameitumia kuinua maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, kisiasa hana umaarufu hata Ukambani ambako Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ana usemi mkubwa ndiposa gavana huyo, aliingia kwenye muungano na chama hicho 2017 ili kurahisisha nafasi yake ya kutetea kiti chake.

Dkt Kituyi naye amekuwa Katibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) tangu Juni 2013. Mbali na hilo, alikuwa Waziri wa Biashara na Viwanda (2002-2007) na pia alikuwa mbunge wa Kimilili, Kaunti ya Bungoma kutoka 1992-2007.

Je, alitumia nafasi hizo kuwafaa wakazi wa eneo la Magharibi anakotoka na Wakenya wa maeneo mengine nchini?

Bi Karua pia amekuwa waziri chini ya utawala wa Rais Kibaki na alilaumiwa pakubwa na wafuasi wa ODM kutokana na uchaguzi tata wa 2007 ila baada ya kuambulia kura 43,000 pekee 2017, angeweka juhudi zake katika kusaka kiti cha ugavana wa Kirinyaga.

Bw Muturi naye tangu atawazwe kuwa Msemaji wa Mlima Kenya licha ya tofauti zilizozuka kuhusu tukio hilo, inaonekana amekosa mvuto kwa kuwa mirengo mbalimbali inaendelea kuchipuka na kuwachanganya zaidi wapigakura kutoka eneo hilo.

Kwa hivyo, ni wazi nia ya wanasiasa hawa wanne wasomi kuungana ni kutumia suala hilo kujisakia nyadhifa aidha katika mrengo wa Dkt Ruto au Bw Odinga kwa kuwa hata wakipendekeza mmoja wao awanie kiti cha Urais, hawana nafasi ya kuingia ikuluni.

You can share this post!

Kero ya umeme kukatika kila mara Kang’oo

WANGARI: Uhifadhi wanyamapori ni turathi kuu kwa vizazi...