Makala

ODONGO: Maafisa wa FKF, klabu wakome kutumia vijana vibaya

July 23rd, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

MNAMO Jumapili Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Robert Muthomi, alijiuzulu baada ya kuandamwa na madai ya jaribio la kufanikisha uhamisho wa mchezaji wa Sofapaka bila kufuata kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Bw Muthomi, yadaiwa alijaribu kufanikisha uhamisho wa mshambuliaji wa Sofapaka, John Avire hadi klabu moja nchini Misri licha ya kwamba mwanadimba huyo bado alikuwa na mkataba wa kuchezea Sofapaka hadi mwaka wa 2020.

Yadaiwa uhamisho wa Avire ungefanikishwa, Bw Muthomi angefaidi kifedha lakini hilo halikutimia baada ya uongozi wa Sofapaka kuutibua na kuwasilisha malalamishi kwa FKF.

Hii tabia ya baadhi ya maafisa kuwahadaa wachezaji kisha kuwatumia kujinufaisha kifedha imekithiri sana na inafaa kukomeshwa.

Ingawa sisemi Bw Muthomi ana hatia, mara nyingi mchezaji ambaye yupo kwenye ubora wake hutafutiwa klabu za kusakatia na maafisa wa timu wanaojifanya maajenti wao, kisha hutia mfukoni kitita kikubwa uhamisho huo unapofaulu.

Cha kusikitisha ni kwamba mchezaji anapokumbwa na matatizo mengi na hata ubora wake kushuka, maafisa hawa huota mabawa na kumwaacha akipambana na changamoto zake kivyake.

Kuna baadhi ya wachezaji nchini waliotumika kwenye biashara hii na makali yao yalipopungua walilazimika kutafuta msaada wa jamaa zao kurejea nchini baada ya kukosa kulipwa mshahara kwa miezi kadhaa., huku maafisa waliofanikisha uhamisho wao hadi mataifa hayo nao wakiwahepa.

Kando na hili la Bw Muthomi, kuna maafisa wa klabu ambao msimu huu wa usajili wanaendelea kuwahadaa vijana wenye nia ya kuchezea timu zao kutoa kitita fulani cha fedha ili wachukuliwe na timu hizo.

Majuma machache yaliyopita, kijana mwenye talanta kutoka shule moja Kaunti ya Homa Bay alisimulia namna alivyoitishwa fedha na afisa mmoja wa Gor Mahia ili ajiunge na timu hiyo baada ya benchi ya kiufundi kupendekeza asajiliwe.

Cha kusikitisha ni kwamba tabia hiyo ilizima ndoto yake kwa sababu hakuwa na fedha hizo, na familia yake maskini haingemudu kiasi kilichoitishwa na afisa huyo. Uongozi wa K’Ogalo bado haujazungumzia suala hili lililoibuliwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii.

Ukweli ni kwamba soka yetu imejaa visa vya ufisadi na ni wakati afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma(DPP) kuelekeza mizani yake kwenye fani hii na kuwashtaki wanaohusika.