Makala

ODONGO: Mvutano wa wanasiasa juu ya IEBC ni njama kuidhibiti

November 2nd, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

JUMA lililopita, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na viongozi wa chama cha ODM, walitofautiana vikali kuhusu gharama ya kuandaa kura ya maoni ili kupitisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa Jumatatu iliyopita katika ukumbi wa Bomas.

IEBC inasema gharama ya kuendesha kura hiyo ya maamuzi ni Sh14 bilioni huku Kinara wa ODM, Raila Odinga akikashifu tume hiyo akisema kiasi hicho ni cha juu mno na inadhihirisha wazi ubadhirifu uliokita mizizi ndani ya IEBC.

Kwa upande mwingine, Naibu Rais Dkt W illiam Ruto na wandani wake nao wamemkemea Bw Odinga wakisema analenga kudhibiti tume hiyo kisiasa ili kumsaidia kuingia Ikulu kwa urahisi 2022.

Kwanza, si siri kwamba viongozi wakuu wa kisiasa nchini sasa wameonyesha wazi kwamba wanalenga kudhibiti IEBC, wakiwa na imani kuwa itawasaidia kuingia Ikulu kwenye uchaguzi wa 2022.

Hii ndiyo maana Dkt Ruto na Bw Odinga ambao ni mahasimu wakuu wa kisiasa wamegawanyika kuhusu usimamizi wa tume hii muhimu.

Pili, ripoti ya BBI inapendekeza makamashina wa IEBC wachaguliwe kutoka kwa vyama vya kisiasa kinyume na sasa hivi ambapo makamishna hao huajiriwa baada ya kupitishwa kwenye michakato kadhaa ikiwemo kuhojiwa na kamati ya Bunge kisha majina kupendekezwa kwa Rais.

Hii itakuwa sawa na uchaguzi wa 1997 ambapo vyama mbalimbali viliruhusiwa kuwateua wawakilishi wao ili wahudumu kama makamishna kwenye iliyokuwa Tume ya Uchaguzi Nchini (ECK) maarufu kama IPPG.

Hata hivyo, ni vyema ikumbukwe kwamba upinzani bado ulishindwa kwenye uchaguzi huo, waliodai ulizingirwa na udanganyifu mkubwa na kupendelea chama cha Kanu.

Kilichoko wazi hapa nchini na Afrika ni kwamba utawala uliopo hutumia njia zote kuhakikisha unasalia mamlakani au kupokeza uongozi kwa kiongozi wanayempendelea kurithi wadhifa huo wa Urais.

Hata haya mabadiliko yanayopiganiwa kupitia BBI yakitekelezwa, bado kutakuwa na viongozi ambao hawataridhika na matokeo ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Inashangaza kwamba Dkt Ruto hivi majuzi alinukuliwa akisema hana tatizo hata Dkt Oburu Oginga (nduguye Raila) akipokezwa wadhifa wa uenyekiti wa IEBC ilhali sasa anapinga uteuzi wa makamishna kutoka kwa vyama vya kisiasa, akitaka walioko sasa waendelee kuhudumu.

Hii inaonyesha kwamba hata pendekezo la BBI likikumbatiwa, upande utakaopoteza bado utalalamika jinsi ilivyo ada.

Aidha, si siri kwamba IEBC jinsi ilivyo kwa sasa inahitaji mabadiliko makubwa kutokana na jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu uliopita.

Tume hiyo ina Mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Mulu pekee. Hii ni baada ya makamishna Roselyn Akombe, Consolata Nkatha, Margaret Mwachanya na Paul Kurgat kujiuzulu huku aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji, Ezra Chiloba naye pia akitimuliwa.

Ingawa kauli ya makamishna wa IEBC kwamba refarenda itakuwa ghali na inaweza kuwa na mashiko, hofu yao ni kwamba kupitishwa kwa BBI kutawafukuza kazini.

Kenya iko na safari ndefu ya kuhakikisha uchaguzi huru unaandaliwa jinsi ilivyokuwa 2002 ambapo upinzani ulikubali matokeo ya urais.