Michezo

ODONGO: Ni haki Oliech kulipwa marupurupu kwa huduma zake Gor

March 5th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

UTATA uliozingira kugoma kwa mshambulizi wa Gor Mahia Dennis ‘The Mennace’ Oliech ulizua mdahalo mkubwa wiki jana, kiini ikiwa ni mwanasoka huyo kutomegewa posho tangu atue kambini mwa K’Ogalo.

Katika taarifa iliyochapishwa magazetini na kuenezwa mitandaoni, ilidaiwa nyota huyo wa zamani wa timu ya Taifa Harambee Stars hakuwa amelipwa ujira wake wa mwezi Januari na sehemu ya fedha za usajili wake.

Maajenti wawili wa mwanasoka huyo ambao ni nduguye walikuja kwa matao ya juu na kupaka tope uongozi wa Gor Mahia kwa kumdharau mwanafamilia wao na kuzichukulia huduma zake vivi hivi klabuni.

Katika mitandao ya kijamii, mashabiki wa K’Ogalo waligawanyika makundi mawili, moja likisimama na Oliech na jingine likipinga kugoma kwake.

Tapo la mashabiki waliokuwa wakipinga walisema Oliech alikosa shukrani baada ya taaluma yake ya soka iliyokuwa imezama kuokolewa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu (KPL). Mashabiki hao walielezea kukerwa na mwanadimba huyo wakimtaka ang’atuke timuni kwa kuwa Gor kwa sasa inajivunia wachezaji waliojaaliwa usakataji kabumbu wa haiba na inaweza kutamba bila uwepo wake.

Baada ya ushindi dhidi ya NA Hussein Dey katika kipute cha Kombe la Mashirikisho, mechi ambayo Oliech hakushiriki, waliotofautiana naye walijimwayamwaya katika kumbi za Facebook na Twitter na kauli ‘Oliech atawaambia watu nini’ ikatrendi.

Kwa upande mwingine, mashabiki walijitokeza na kuunga mkono mshikilizi huyo wa rekodi ya mfungaji bora nchini na kuitaka Gor Mahia kumpa haki yake. Wengi wao walisikitikia aliyokuwa akiyapitia Oliech na kutoa wito alipwe.

Usimamizi wa Gor Mahia ukiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Ludovic Aduda nao ulijitokeza kukanusha kwamba wanadaiwa fedha zozote na mwaajiriwa wao. Aduda kupitia mahojiano na Taifa Leo alisema wametii na kuheshimu mkataba wao na Oliech huku akifichua kuna watu fulani wanaochipuza mambo yasiyo kweli ili kutatiza udhabiti wa K’Ogalo.

Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba liwalo na liwe ni haki ya straika huyo kulipwa mshahara, marupurupu na fedha zozote anazodai mabingwa hao mara 17 wa KPL. Tabia ya kila mara ya baadhi ya klabu kutia saini mikataba na wachezaji kisha kuwageuka ni ukosefu wa maadili na ustarabu.

Madai ya mashabiki kwamba Oliech anafaa kuishukuru Gor kwa kuifufua taaluma yake pia hayana msingi. Gor Mahia na Oliech wanahitajiana ndiposa kila upande lazima uwajibike na kutekeleza wajibu wake kulingana na mkataba wao.

Kwa kweli, hakuna mtu ambaye atafurahikia kufanya kazi yoyote bila kulipwa fedha akiwemo Oliech. Ingawa hivyo, iwapo itabainika madai hayo yalikuwa uongo, naomba Oliech atimuliwe kwa kuichafulia jina klabu kubwa kama Gor Mahia.