Maoni

ODONGO: Ni kinaya Ruto kushambulia mahakama aliyosifu baada ya kura

January 4th, 2024 2 min read

Na CECIL ODONGO

Kauli ya Rais William Ruto kuwa atawafyeka wakora ambao wanatumia mahakama kupiga breki miradi yake ya maendeleo haifai kutoka kwa kiongozi wa taifa.

Rais Ruto alisema kuwa kisu cha ulinzi alichokabidhiwa si cha kukata mboga bali cha kuwafyeka wale ambao wanatatiza agenda yake ya maendeleo.

Juzi tu Rais ameendelea kukashifu Idara ya Mahakama akionekana kuwalenga majaji ambao wamekuwa wakiamua kesi kuhusu sera ambazo serikali inapanga kutekeleza.

Mwanzo, inashangaza kuwa sasa kiongozi wa taifa na wandani wake wameelekeza nguvu zao kukashifu idara ya mahakama ilhali ni mwaka moja uliopita walikuwa wakiisifia.

Mahakama ilimiminiwa sifa kedekede na Rais kama idara huru ambayo iliwajibikia kazi yake ipasavyo baada ya kudumisha ushindi wa Kenya Kwanza.

Punde tu baada ya kutwaa mamlaka, Rais alionekana ‘kushukuru’ korti na hata akawaapisha baadhi ya majaji wa mahakama kuu na rufaa ambao mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alikataa kuwaapisha.

Kauli za rais za kuimiminia sifa mahakama ziliendelea kushamiri na wakati mmoja ilidhaniwa ameiteka idara hiyo ya mahakama.

Hata alipokuwa akiekea bungeni kutoa hotuba yake ya kwanza baada ya uchaguzi wa 2022, Jaji Mkuu Martha Koome alikashifiwa kwa kuwa kati ya waliotia foleni kumlaki Rais katika majengo ya bunge.

Je, nini imebadilika sasa kiasi kuwa kiongozi wa nchi anatishia idara ya mahakama?

Hata Rais na wandani wake wanafahamu kuwa sera za ushuru na Sheria ya Fedha ya 2023 haichangamkiwi na raia.

Kutumia vitisho zaidi dhidi ya majaji hakutabadilisha fikira za raia ambao tayari wanaumizwa na sera hizo hasi.

Rais Ruto anastahili kukumbushwa kwa viongozi ambao waliwahi kutumia kifua dhidi ya wananchi, wote hawakufanikiwa uongozini.

Hata marehemu Rais Daniel Arap Moi alijaribu kuzima mfumo wa vyama vingi nchini lakini wito na nguvu za raia zikamzidi.

Ni dhahiri kuwa Wakenya wamechoka na serikali hii kutokana na uongo unaoenzwa na viongozi wake ilhali hakuna kazi yoyote ambayo inaendelea.

Kuwatishia majaji hakutaleta maendeleo nyanjani.