Makala

ODONGO: ODM iheshimu washirika wake katika NASA, bado itawahitaji

July 31st, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha ODM hakifai kudhalilisha vyama vingine kwenye muungano wa NASA kwa sababu bado kitahitaji washirika wa kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

ODM kupitia Katibu wake Edwin Sifuna, wikendi iliyopita ilimkemea kwa maneno makali mno kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyedai alikuwa na mkataba wa kisiri na Kinara wa upinzani Raila Odinga.

Bw Musyoka alidai Bw Odinga mnamo 2017 aliahidi kumvumisha kama mwaniaji wa Urais 2022 baada ya wawili hao kushirikiana kisiasa tangu 2013

ingawa juhudi zao za kutwaa urais hazikufanikiwa.

Kuwepo kwa mkataba kama huo au kukosekana kwake hata hivyo si hoja kwa sababu mazingira ya siasa hubadilika kila mara. Mikataba pia huvunjwa.

Hata hivyo, hiyo haikuwa sababu tosha kwa Bw Sifuna kumdhalilisha Bw Musyoka akirejelea utikitimaji wake kwenye masuala muhimu kitaifa na kupungua kwa umaarufu wake hasa eneo la Ukambani.

Ingawa Bw Odinga hajatangaza wazi kwamba analenga kuwania Urais, semi za wandani wake, akiwemo kakake Dkt Oburu Oginga zinaashiria huenda atakuwa kinyang’anyironi 2022 tena kujaribu bahati yake kwa mara ya tano.

Hivyo basi, huenda akahitaji uungwaji mkono wa Wiper na hata vyama vya Ford Kenya, ANC, CCM na vyama vingine ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu.

Kile Bw Sifuna anafaa kufahamu ni kwamba, ODM haiwezi kumpokeza Odinga fungo za ikulu isiposhirikiana na viongozi wengine nchini.

Licha ya kwamba kinara huyo wa upinzani yupo kwenye ukuruba wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta, si siri kwamba hana umaarufu wa kutosha katika eneo la Kati ikilinganishwa na Naibu Rais Dkt William Ruto eneo hilo. Hivyo, basi hana uhakika atapata kura nyingi eneo hilo kuliko maeneo wanakotoka washirika wake waliomuunga mkono 2017.

Ndio maana bado Bw Odinga atahitaji kudumisha umaarufu kwenye ngome yake na ya washirika wake wa kisiasa kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Ikiwa ODM ipo kwenye ushirikiano wa kisiasa na Jubilee, basi haifai waone wivu Wiper na hata chama kingine pia kikifuata mkondo huo wa kisiasa.

Aidha, inafaa kutathmini kwa makini iwapo iliahidi washirika wake sehemu ya mgao wa Sh4.1 bilioni za vyama vya kisiasa badala ya kulazimika kukanusha suala hilo mara kadhaa. Tayari ANC imetishia kuelekea mahakamani ikisema inastahili kupata sehemu ya fedha hizo.

Hata hivyo, mienendo ya ODM na hata kuvunjwa kwa mikataba ya kisiasa miaka ya nyuma kunafaa kuwe funzo kwa Wiper, Ford Kenya, ANC na hata mrengo wa Tangatanga kwamba kila chama lazima kijiimarishe na kushinda viti vingi maeneo mbalimbali ili kudhihirisha umaarufu wa kinara wake.