Makala

ODONGO: ODM imejinusuru kwa kufanya uteuzi wa kweli

October 5th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

CHAMA cha ODM kimedhihirisha kwamba kimeanza kukumbatia mabadiliko ya kweli kutokana na jinsi kilivyoandaa uteuzi wa mgombeaji wa kupeperusha bendera yake katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni wiki iliyopita.

Kwa mara ya kwanza ODM iliandaa mchujo ambao haukusheheni ghasia au vurugu jinsi ambavyo imekuwa ikishuhudiwa kuelekea uchaguzi mkuu au michujo ya chaguzi ndogo.

Licha ya matatizo madogo madogo ya majina ya wanachama kukosekana katika sajili ya wapiga kura iliyotumika, matokeo yalionyesha wazi kwamba Omar Boga ndiye alikuwa kipenzi cha raia eneo hilo.

Bw Boga alikuwa diwani wa wadi ya Bongwe-Gombato kupitia ODM kabla ya uchaguzi mkuu uliopita. Mnamo 2017, alishindwa na marehemu Suleiman Dori kwenye mchujo wa chama na pia katika uchaguzi mkuu alipowania kama mgombea wa kujitegemea.

Hata mpinzani wa Bw Boga, Nicholas Zani ambaye alijizolea kura 530 pekee katika vituo 61, hakulalamikia matokeo hayo wala kuelekea kortini kuyapinga.

Yafaa ODM itumie mchujo huo wa Msambweni kama msingi wa kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2022 na bila shaka itarejelea umaarufu wake jinsi ilivyokuwa 2007, iliposhinda viti 99 vya ubunge kati ya vyote 208 wakati huo.

ODM ilianza matayarisho kwa kura ya 2022 kwa kuteua bodi mpya ya uchaguzi na pia wanachama wapya wa kamati ya nidhamu chamani mnamo Agosti mwaka huu.

Bodi hiyo mpya chini ya mtaalamu wa kisheria Catherine Mumma ina kibarua kigumu kuhakikisha kwamba ufanisi ulioshuhudiwa katika eneobunge la Msambweni, unafanyika pia kwenye mchujo wa chama kabla ya kura ya 2022.

Katika chaguzi za 2013 na 2017 baadhi ya wakuu chamani walivuruga mchujo wa ODM huku madai yakizuka kwamba waliokuwa wakilipa pesa nyingi ndio walipewa tiketi bila kujali umaarufu wao miongoni mwa raia.

Hii ilisababisha chama kupoteza viti muhimu katika ngome yake ya kisiasa kwa wawaniaji huru au wa vyama vingine.

Wabunge Mohammed Ali (Nyali) na Peter Masara (Suna Magharibi) ni kati ya walioshiriki mchujo wa ODM na kunyimwa tiketi ya chama kwa njia tatanishi lakini hatimaye wakashinda kama wawaniaji wa kujitegemea.

Katika eneobunge la Muhoroni, utata wa mpeperushaji wa bendera ya chama kati ya mbunge wa sasa Onyango K’oyoo na Mbunge wa zamani Profesa Ayiecho Olweny uliendelea hadi siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

Majaji wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga mnamo Agosti 6 walitoa uamuzi wa kubatilisha kupokezwa kwa tiketi kwa Bw Olweny na kuagiza Bw K’oyoo aruhusiwe kuwania baada ya kukata rufaa kuhusu uamuzi uliotolewa na korti za chini.

Matukio kama haya sasa yatazikwa kwenye kaburi la sahau iwapo ODM itakuwa ikiendesha chaguzi zenye uwazi na huru na kuzingatia mapenzi ya raia.

Pia Kiongozi wa ODM Raila Odinga amenukuliwa akisema mchujo wa 2013 na 2017 ulivurugwa ndiyo maana idadi ya wabunge wa chama waliochaguliwa ilishuka hadi 76.

Vilevile ODM hata iwapo itaingia kwenye Muungano na vyama vingine, haifai kutosimamisha wawaniaji wake kwenye chaguzi katika maeneo ambayo ina umaarufu kisiasa.

Katika eneobunge la Kitutu Chache Kusini Kaunti ya Kisii ODM ilimuunga mkono mgombeaji wa Ford Kenya Richard Onyonka na kumtema Samwel Omwando kwenye kura iliyopita.

Hatua hiyo si haki na inadhihirisha kwamba chama hakiwathamini wagombeaji wake.