ODONGO:  Polisi wakome kutumia Covid-19 kuendeleza ufisadi

ODONGO: Polisi wakome kutumia Covid-19 kuendeleza ufisadi

Na CECIL ODONGO

HUKU Waziri wa Afya Mutahi Kagwe anapojikaza kila siku kushawishi Wakenya kutii kanuni zilizowekwa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, mwenzake wa Usalama Fred Matiang’i anapasa kuweka bidii kuhakikisha kuwa juhudi hizi hazivurugwi na maafisa wa polisi.

Kati ya kanuni zilizotangazwa na serikali ni kafyu, marufuku ya kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kwale na Kilifi, baa zote nchini kufungwa, watu kutokusanyika wengi mahala pamoja, kuvaa maski miongoni mwa zingine.

Katika kuhakikisha kuwa kanuni hizi zinazingatiwa na wananchi, polisi wana jukumu kubwa na wanatarajiwa kutekeleza wajibu huu kwa kujitolea ili kuhakikisha wananchi hawajiweki kwenye hatari ya kuambukizwa ama kusambaza virusi vya corona.

Lakini inasikitisha kuwa badala ya kutambua hatari ya ugonjwa huu kwa wananchi na hata wao wenyewe, baadhi ya maafisa walaghai wa polisi wamegeuza kanuni hizi kuwa njia yao ya kukusanya hongo na kuhatarisha zaidi maisha ya Wakenya.

Kunao raia wengi ambao wameelezea kuhusu jinsi polisi wanavyowakamata wanaopatikana wakivunja kanuni hizi na kuwarundika kwenye magari yao na seli za polisi bila kutambua hatari ya kuambukizana virusi vya corona watu wanaposongamana.

Polisi hawa wanatengeneza mazingira haya ili kuwatia wasiwasi washukiwa wa kuambukizwa virusi, kwa lengo la kuwataka walipe hongo ndiposa waachiliwe huru.

Baadhi ya maafisa nao wanashirikiana na wenye mabaa hasa jijini Nairobi ambapo wanawaruhusu kuendelea kuuza pombe vilabuni baada ya kulipa hongo kwa polisi.

Wengine wanapowakamata watu wakiwa wamekusanyika pamoja wanawatisha kuwapeleka karantini kama hawatatoa rushwa.

Matukio haya ni ya kusikitisha kwani yanahujumu juhudi za serikali za kuzima ueneaji wa virusi vya corona.

Waziri Matiang’i anafahamika kwa kutumia mbinu kali kuhakikisha anachotaka kifanyike kimetimia, na ndiposa inazua maswali kuhusu ni kwa nini amekosa kuhakikisha polisi wanaheshimu sheria na kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya corona kwa kufanya kazi yao kwa uwazi na kujitolea.

Wananchi wamekuwa wakipiga ripoti kuhusu vilabu vinavyokiuka sheria lakini wakuu husika wa polisi wanapuuza ripoti hizo kutokana na mchuzi wanaopata kutoka kwa wamiliki.

Ni makosa sana kwa polisi kuhusika katika kuhatarisha maisha ya Wakenya, na ni kwa sababu hii ambapo Dkt Matiang’i hana budi kukaza kamba na kuhakikisha maafisa wote wanaheshimu sheria.

You can share this post!

Sikujua mkataba niliotia saini utageuzwa, sasa nitauvunja...

Polo aona moto kuchezea maski

adminleo