Makala

ODONGO: Raila awe Rais kutokana na sera wala si kutuzwa

August 12th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga apasa kuwa Rais 2022 kutokana na jinsi anavyozinadi sera zake na kuwaridhisha Wakenya na wala si kutunukiwa tu kutokana na jitihada zake za ukombozi wa pili na kupigania mfumo wa ugatuzi.

Wikendi iliyopita, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe akihojiwa na kituo kimoja cha habari nchini, aliwataka Wakenya wajitayarishe kwa Urais wa Bw Odinga 2022.

Bw Murathe alifichua kwamba, Bw Odinga atahudumu tu kwa muhula mmoja kisha kupisha kizazi cha vijana kutwaa wadhifa huo 2027.

Sifa za Bw Odinga za ukombozi ni wazi kwa anayefahamu historia nchini ila si vyema apokezwe wadhifa huo kama zawadi ilhali kuna wanasiasa walioshiriki ukombozi huo lakini hawakutuzwa miaka ya nyuma.

Marehemu Kenneth Matiba na George Anyona walipigania ukombozi wa pili 1992 lakini walipata kura ambazo hazikutosha kuwasaidia kumshinda marehemu Rais Daniel Arap Moi. Martin Shikuku pia alikuwa debeni mnamo 1997 lakini hakuhurumiwa na kupokezwa kura nyingi licha ya kwamba pia alikuwa mtetezi wa wanyonge.

Vilevile, kauli ya Bw Murathe ambaye ni mbunge wa zamani wa Gatanga haiafiki kwa kuwa kuna uhakika gani Bw Odinga atahudumu muhula moja pekee kisha kung’atuka na kumwachia kiongozi mwingine?

Barani Afrika, viongozi huwa malaika na huahidi kuongoza kwa mihula miwili lakini muda unapotimia wa kuondoka, wao hukwamilia mamlakani na mara nyingi hulazimishwa tu kutii baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Marais Paul Biya (Cameroon), Idris Deby (Chad) na Ismael Guelleh wa Djibouti ni kati ya viongozi walioko mamlakani hadi leo baada ya kubadilisha katiba na kufutilia mbali hitaji la kuhudumu mihula miwili.

Afrika Mashariki na Kati, aliyekuwa Rais wa Burundi marehemu Pierre Nkurunziza alikataa kuondoka mamlakani mnamo 2015 licha ya kuhudumu kwa mihula miwili. Msimamo wake ulizua maandamano makubwa na mauti ya raia lakini aliushikilia hadi akabadilisha na akaendelea kuongoza hadi kifo chake.

Pia, kuna mfano wa Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ambaye alikuwa katika upinzani na mwanaharakati aliyeahidi mabadiliko mengi mazuri kwa raia.

Cha kushangaza ni kwamba, siku chache baada ya kushinda urais, aliwateua jamaa zake katika nyadhifa mbalimbali. Hii inaonyesha viongozi wa Afrika hawaaminiki na hakuna anayejua yatakayofuatia baada ya wao kushika hatamu za uongozi.

Ingawa Marais Wakenya wamekuwa wakiheshimu utawala wa mihula miwili, kuna uhakika gani Bw Odinga atafuata mtindo huo?

Bw Odinga ni kiongozi mzalendo ambaye amejaribu bahati yake mara nne debeni japo hakufanikiwa. Hata hivyo, hii haimanishi watu watamkataa 2022 kwa sababu eti Bw Murathe amependekeza Urais wake mapema kwa msingi wa jitihada zake za ukombozi miaka ya nyuma.

Kama kiongozi mkakamavu, Bw Odinga anayejivunia uungwaji mkono kote nchini, anafaa kujiuza kwa sera zake badala ya kuonekana kama aliyelemewa na mkosi wa kuanguka kura kila mara za urais na anayefaa kufanyiwa hisani na kupokezwa wadhifa huo bila kutokwa jasho.