ODONGO: Raila si kikwazo kwa wabunge kuonana na rais ikulu

ODONGO: Raila si kikwazo kwa wabunge kuonana na rais ikulu

NA CECIL ODONGO

Baadhi ya wabunge wa Chama cha Jubilee walinishangaza kwa kudai kwamba kinara wa ODM Raila Odinga amewazuia kuonana na Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala cha Jubilee.

Wanasiasa hao ambao ni wa kundi la Tangatanga, wengi wao wa kike ambao pia wapo kwenye kundi la Inua Mama Jenga Taifa walisema kwamba hawajaweza kumwona Rais tangu salamu za maridhiano kati yake na Bw Odinga maarufu kama ‘Handisheki’ mwaka uliopita.

Kauli hii inashangaza na huenda isiwe na ukweli wowote ikizingatiwa kwamba wabunge hawa ni wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye amekuwa akishirikiana bega kwa bega na Rais kuendesha serikali tangu waingie mamlakani mwaka wa 2013.

Swali ni je kwa nini wasitumie urafiki wao na Naibu Rais kumshawishi azungumze na Rais ili aandae mkutano nao badala ya kusimama majukwaani na kulia kana kwamba wao siyo sehemu ya serikali inayoongoza?

Pili, Dkt Ruto amenukuliwa mara kadhaa akisema kama msaidizi wa Rais, anajukumu la kuhakikisha kwamba manifesto ya Jubilee inatekelezwa kikamilifu na miradi ya maendeleo waliyoahidi inatimizwa. Je,viongozi hawa wamewasilisha masuala hayo ninayoaamini yanagusia maendeleo kwa Naibu Rais?

Je, Naibu Rais ameshindwa na kuwaeleza kwamba ni Rais pekee ndiye ana uwezo ya kuyashughulikia maswala hayo??Hata kama inaonekana wazi kwamba huenda Rais amebadilika tangu aingie kwenye ndoa na Bw Odinga, wabunge hawa pia wamechangia kubadilika kwake na nia ya kuu ni kumwona Rais kutokana na ajenda za kisiasa wala si masuala ya maendeleo.

Kinaya ni kwamba mara si moja, wamekuwa kwenye vyombo vya habari wakipinga sera zake na masuala yaliyomo kwenye muafaka ulioafikiwa mwezi Machi mwaka jana pamoja na jopokazi lililobuniwa na Rais na Bw Odinga maarufu kama BBI.

Vilevile Rais mwaka jana alijibu wabunge hawa ambao wengi wao wanatoka maeneo ya Bonde la Ufa na Kati kwamba wanafahamu njia ya kupatana naye ila hatashawishika kuingia kwenye mitego yao ya kisiasa na akawataka kutilia maanani huduma kwa waliowachagua badala ya kuzunguka taifa lote wakipiga siasa.

Badala ya kulalama kwamba Bw Odinga amekuwa kikwazo kwao kumwona Rais, wanafaa kutupilia mbali kiburi chao na kuonana na kinara huyo wa ODM kisha wamshawishi apendekeze Rais awe na kikao nao kwa kuwa ni dhahiri uhusiano wao wa karibu Dkt Ruto haujawawezesha kufanikisha jitihada zao za kuonana na kiongozi wa nchi.

Hata hivyo naamini matamashi ya wanasiasa hawa hayana mashiko na walidhamiria kumshambulia Bw Odinga jinsi wanavyofanya kila mara.

You can share this post!

NGILA: Dunia isipodhibiti teknolojia za #Deepfake,...

WANGARI: Kibra waheshimu Okoth kwa kuchagua mchapakazi

adminleo