Makala

ODONGO: Tume ya NCIC inapasa kuvunjiliwa mbali sasa

August 8th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

NI jambo la kusikitisha kwamba makamishina wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) wamekimya huku vifo vikiendelea kutokea kutokana mapigano ya kikabila kati ya jamii mbili hasimu katika kaunti za Narok na Nakuru.

Katika kisa cha Olposimoru, Narok Kaskazini, makabiliano yalichacha kati ya jamii mbili hasimu kutokana na mauaji ya vijana wawili waliyokuwa wakilisha mifugo. Pia wizi wa mara kwa mara wa mifugo umetajwa kama kiini cha ghasia hizo.

Kwenye tukio la pili, watu watatu waliuawa eneo la Marioshoni, katika mpaka wa Kaunti za Nakuru na Narok. Jamii mbili za eneo hilo nazo zinazozania umiliki wa vipande vya ardhi.

Kwenye visa vyote viwili majeruhi kadhaa yameripotiwa huku polisi wakilazimika kuingilia kati na kuzima mapigano zaidi kati ya jamii hizo hasimu.

Hata hivyo, si siri kwamba huenda wanasiasa kutoka pande zote wanahusika na visa vya uchochezi na kwa njia moja au nyingine wamechangia ghasia hizo kichinichini.

Mojawapo ya jukumu la NCIC kikatiba ni kusuluhisha uhasama kati ya makabila yanayozozana kwa njia ya amani, tena bila kupendelea upande wowote na kwa mchakato unaozingatia ubinadamu.

Tume hiyo pia ina wajibu wa kuhakikisha kuna utangamano na umoja wa kitaifa, kushughulikia dhuluma za kihistoria zinazozua vita vya kijamii kati ya majukumu mengine.

Ingawa hivyo, NCIC inayoongozwa na kasisi mkongwe Samuel Kobia, haionekani kutikiswa na vita vya kikabila Narok na Nakuru wala haijazungumza chochote kuhusu ghasia hizo.

Makamishina wa tume hiyo pia hawajazuru maeneo yaliyoathirika kujionea kiwango cha uharibifu wa mali uliotekelezwa huku hali ikizidi kuwa mbaya iwapo serikali itazembea kudhibiti mapigano hayo. Mbona wamelala kazini na hii ni sehemu ya wajibu wao?

Hali hii inazua swali kuwa je, wajibu wa NCIC pekee ni kuwasukama seli viongozi wanaotoa matamshi ya uchochezi katika majukwaa ya kisiasa pekee?

Badala ya kukimya NCIC ingekuwa mstari wa mbele kuwatambua wanasiasa wanaochochea mapigano hayo kisha kutangamaza majina yao hadharani na kuwashtaki mahakamani. Hata hivyo, kimya chao huenda kikawapa wanasiasa hao msukumo wa kuendelea kuchochea vita.

Kile ambacho kimeonekana katika juhudi za kuhakikisha kuna amani maeneo hayo ni serikali ya kaunti ya Nakuru kuweka kafyu ya saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni katika maeneo ya Njoro, Mau Narok and Elburgon .

Kama tume iliyojukumiwa kuhakikisha umoja na amani, NCIC ndiyo ingekuwa mstari wa mbele kupigia upato badala kuachia serikali za kaunti na wanasiasa jukumu hilo.

Ikizingatiwa kwamba NCIC ilibuniwa 2008 baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007, tume hiyo ingekuwa imeweka msingi na kupata mamlaka zaidi kutoka kwa serikali iwapo kuna mwanya au vizingiti vinavyozuia utendakazi kuwa imara miaka hii yote.

Wakenya wataendelea kuumia iwapo kazi ya NCIC itakuwa ni kuwaonya wanasiasa wachochezi na kushauri serikali ichukue hatua dhidi yao bila tume hiyo kuchukulia majukumu yake kwa uzito na kupata mamlaka zaidi.

Miaka 12 baada ya kuundwa kwake, NCIC haijaafikia chochote ya kuwaridhisha Wakenya kwamba ni tume muhimu ambao makamishina wake wanalipwa na fedha za mlipa ushuru.