Makala

ODONGO: Viongozi hawafanyii raia hisani kutekeleza miradi

December 14th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

AIBU iliyoje kwa viongozi waliochaguliwa kuzozania mradi wa maendeleo ilhali wana hazina za kutumia kuanzishia wananchi miradi mingi tu katika maeneo yao ya uwakilishi.

Wiki jana, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Homa Bay, Gladys Wanga, na Mbunge wa Rangwe, Lilian Gogo, walizindua mradi mmoja wa ujenzi wa barabara ya Olare-Mariwa na ule mradi wa maji wa Luaho.

Bi Wanga alipozuru mradi alidai mradi ulipenya tu baada yake kufika katika afisi za Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara za Mashinani (KRRA) na kushawishi asasi hiyo kuanza ujenzi.

Kwa upande mwingine, Bi Gogo naye alidai ni yeye alishawishi serikali kuu kuuanzisha mradi huo katika eneobunge lake, akimkemea Bi Wanga kwa kuijitafutia umaarufu wa kisiasa.

Tukio la wabunge hao kuzozania mradi moja si geni; kuna magavana na wabunge ambao wamekuwa wakivutana mara kwa mara kuhusu miradi katika maeneo yao.

Hata hivyo, swali kuu ni kwanini viongozi wazozanie miradi ilhali wana hazina za kufadhili maendeleo ya kutosha katika miaka mitano yao uongozini?

Bi Gogo ana Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF); Bi Wanga ana hazina iliyotengewa wawakilishi wa kike maaarufu NGAAF.

Je, viongozi hawa wawili wametumia fedha zote katika hazina yao kwenye miradi ya kutosha, kiasi kwamba sasa wanavutania ile iliyoanzishwa na serikali kuu?

Katika ripoti ya kampuni ya Infotrak majuzi kuhusu wabunge wachapa kazi, Rangwe iko nambari 100 kati ya maeneobunge yote 290.

Inadhihirisha kwamba eneobunge hilo halijapiga hatua kimaendeleo ipasavyo ilhali Bi Wanga na Bi Gogo wanazozania miradi ya serikali kuu badala ya kuanzisha yao.

Wabunge wafahamu kuwa hawafanyii raia hisani wanapozindua miradi ya CDF ama ya serikali kuu kwa sababu ni haki ya kila mlipa ushuru kuhudumiwa na utawala uliopo.

Pili, ni wazi kuwa kiini cha uhasama kati ya viongozi ambao hung’ang’ania miradi ni siasa za 2022.

Wengi wao wanataka kujihusisha na hata miradi ambayo hawajatekeleza ili wapate mnofu rahisi wa kutupia raia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, kujifanya eti wao ni wanasiasa wachapa kazi.

Bi Wanga tayari ametangaza azma ya kuwania kiti cha ugavana 2022 na huenda amegutuka kuwa hajafanya maendeleo yoyote ya maana kupitia pesa za NGAAF; ndiposa anadakia miradi isiyo yake.

Naye Bi Gogo ambaye analenga kutetea kiti chake amekataa kuketi kitako akiona kiongozi mwingine akijihusisha na miradi yake, na kufanya raia wamwone kama mzembe.

Yote tisa, wanasiasa wetu wafahamu kwamba nyakati hizi raia wamepevuka na wanajua miradi iliyoanzishwa na serikali kuu na ile inayoendeshwa na NGAAF au CDF.

Pia wakazi wengi siku hizi huwa wanaangalia utendakazi wa kiongozi kabla ya kumchagua bila kujali umaarufu wa chama katika eneo.

Hii ndiyo maana Bi Wanga na Bi Gogo wamegutuka na kugundua kuwa umaarufu wa chama cha ODM katika eneo hilo hautawasaidia wasipowajibikia raia kupitia miradi ya maendeleo.