MakalaMichezo

ODONGO: Viongozi wa soka wawe vielelezo bora na wenye maadili

January 15th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

ZIMWI la vurugu katika fani ya soka, wiki jana lilirejea na kupaka tope kwa mara nyingine mchezo huo unaohusudiwa na wananchi wengi nchini.

Ghasia hizo zilizotokea wakati wa pambano la Ligi Kuu nchini (KPL) kati ya AFC Leopards na Nzoia Sugar ugani Kenyatta, Kaunti ya Machakos mara hii hazikuhusisha mashabiki tu bali afisa wa ngazi ya juu katika klabu, hali inayozidi kutia doa maadili ya baadhi ya viongozi wa klabu mahiri nchini kama Ingwe na Gor.

Viongozi hao huchaguliwa katika nyadhifa hizo ili kuhudumia klabu kwa uwazi, uzalendo na kuwa kielelezo bora kwa mashabiki ili kuvutia wadhamini na kuziwezesha timu zao kutoa ushindani ligini.

Katibu Mkuu Mpanga ratiba wa AFC Leopards Timothy Lilumbi na mashabiki wa timu hiyo walijitosa uwanjani baada ya mtanange huo wakiwa wamepandwa na mori na kumpa kichapo kikali refa wa mechi hiyo George Mwai.

Kiini cha kichapo hicho kikali ni hatua ya msimamizi huyo kulikumbatia bao safi lililofungwa na Nzoia Sugar katika dakika za jioni za mchuano huu na kupelekea timu hizo kuagana sare, matokeo ambayo yalikuwa kinyume na matarajio ya mashabiki wa Ingwe.

Ingawa kama kawaida Shirikisho la soka nchini (FKF) lilijitokeza na kukemea tukio hilo kwa kinywa kipana na hata kuanzisha uchunguzi kulihusu, ni wazi kama mchana wa jua kwamba hatujajifunza kutokana na matukio sawa na hayo siku za nyuma.

FKF na KPL zinafaa kukaza makali ya sheria zilizopo zikilenga kurejesha nidhamu katika soka ili kuyanusuru maisha ya mashabiki na wasimamizi wa mechi ambao huchangia pakubwa ufanisi wa mchezo huo kwa nija moja au nyingine.

Zahama katika ulingo wa soka hapa nchini si jambo geni na hata zimewahi kusababisha vifo vya wengi ingawa katika muda wa miaka mitatu iliyopita visa hivyo vimepungua sana.

Japo uongozi wa AFC Leopards umetangaza kwamba Bw Lilumbi amesimamishwa kwa muda kuhudumu katika wadhifa huo ili kupisha uchunguzi, tabia aliyoionyesha haifai kuvumiliwa katika mchezo wa soka enzi hizi.

Itakuwa furaha na adhabu tosha iwapo atatozwa faini kubwa au kupigwa marufuku kwa muda mrefu kabla ya kuruhusiwa kujihusisha na masuala ya soka tena.

Wasimamizi wa mechi nao wanafaa kumakinikia majukumu yao ili kuzuia kutoa maamuzi yanayoibua utata yanayopendelea timu moja. Hii itafanikiwa tu iwapo watapokea mafunzo ya mara kwa mara na pia kuiga na kutazama jinsi ligi za ughaibuni zinavyoendeshwa.