Bambika

Oga Obinna ashangaa kuambiwa ustaa wake hauruhusu kuishi nyumba ya kupanga

February 25th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MCHEKESHAJI Steve Thompson Maghana almaarufu Oga Obinna, ameshangaa baada ya kuambiwa ni makosa makubwa kwa mtu maarufu kama yeye kuishi katika nyumba ya kupanga.

Shabiki mmoja kwa jina Kenzy Kenzia Abba, alimwachia ujumbe mchekeshaji huyo kwenye ukurasa wa Instagram akisema haelevi ni vipi msanii huyo wa jina kubwa anavyotumia pesa ‘kiholela’ kwa kulipa kodi ya nyumba jijini Nairobi.

“Baba mzuri… anayetumia pesa vibaya kwa nyumba za kukodi,” akaandika Abba.

Lakini Oga alijibu kwa vijembe akitania kuwa hakuwa anajua kuishi kwa nyumba ya kupanga kungeudhi mashabiki wake.

Aliongeza kuwa anatafakari pengine kuhamia mashambani kuishi katika nyumba yake ambayo ameijenga kijijini kwao.

“Wueh!! Acha niache kukodi (nyumba). Niishi kwangu penye nimejenga ushago kwa kuwa nawakosea sana. Samahani sio kupenda kwangu,” akaandika Oga.

Kauli yake ilipata shavu kwani mashabiki wake wengine waliimuunga mkono kikamilifu.

Lakini wengine walishikilia kuwa jamaa wetu ni tajiri wa kutosha kumiliki nyumba na si wa kuishi kwa kupanga nyumba akitakiwa kulipa kodi kila mwezi.

“Naweza kukuuzia nyumba,” akasema shabiki Mintos.

Aliyechekesha zaidi ni Ndogo Charlie aliyeshangaa jinsi Oga atakavyokuwa akisafiri kila siku kutoka mashambani hadi jijini Nairobi kwa shughuli za kikazi.

“Kuanzia leo anza kusafiri kutoka mashambani na kuja kazi jijini Nairobi,” akasema Charlie.