Ogallo aapa kufukuzia kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Grand Prix ya taekwondo

Ogallo aapa kufukuzia kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Grand Prix ya taekwondo

Na GEOFFREY ANENE

MWANATAEKWONDO Faith Ogallo analenga juu katika mchezo huo baada ya kutangaza kuwa anataka kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki mashindano ya donge nono ya Grand Prix.

Katika mahojiano Jumanne baada ya kuwasili kutoka Senegal ambako Kenya ilikamilisha mashindano ya Bara Afrika katika nafasi ya saba kati ya mataifa 36 kwa kuzoa medali tatu za shaba, Ogallo, ambaye atawakilisha Kenya kwenye Olimpiki mwezi ujao, alisema anatafuta kuweka historia hiyo.

Mshindi huyo wa medali ya fedha kwenye michezo ya African Games alipoteza pembamba katika nusu-fainali 4-3 dhidi ya Mmoroko Koutbi Sabah na kuambulia nishani ya shaba mjini Dakar mnamo Juni 5-6.

“Nilicheza vyema kwa sababu hatukuwa tumeshiriki mashindano yoyote kwa muda mrefu kutokana na janga la virusi vya corona. Nashukuru Mungu kwa kupata medali, ingawa sikupata matokeo niliyoyataka. Medali hii itanipa motisha ninapoelekea Olimpiki mjini Tokyo,” Ogallo alisema na kufichua kuwa alikuwa amelenga medali ya fedha ama dhahabu mjini Dakar.

Alisema kuwa mashindano ya Dakar yalikuwa yake ya mwisho kabla ya Olimpiki mnamo Julai 23 hadi Agosti 8.

“Kutokana na masharti ya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19, sasa nitaelekea kambini Kasarani. Nimeruhusiwa kuenda nyumbani siku kadhaa nipakie kila kitu nitahitaji kwa sababu hakuna kutoka kambini ukishaingia,” alifichua mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kibabii.

Ogallo alieleza Taifa Leo kuwa mipango yake baada ya Olimpiki ni kushiriki mashindano ya dunia mjini Wuxi ambayo yaliahirishwa kutoka mwezi uliopita hadi Oktoba kwa sababu ya Olimpiki.

“Natumai kuenda katika mashindano ya dunia baada ya Olimpiki. Lengo langu ni kufika katika mashindano ya kifahari ya Grand Prix na ninaweza kufanya hivyo kwa kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano mengi na kupata kuorodheshwa katika nafasi nzuri kwenye viwango vya ubora duniani,” alisema.

Kushiriki Grand Prix, aliongeza, pia kutamsaidia kupata uzoefu zaidi na ujuzi na hata tiketi ya kushiriki Olimpiki zijazo moja kwa moja akishinda kitengo chake.“Nataka kuandikisha historia kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Grand Prix,” alisema.

Kocha wa timu ya taekwondo Linus Marangu alisema kuwa kwa jumla matokeo ya Kenya mjini Dakar yalikuwa mazuri kwa sababu Ogallo hakuwa amefikia kiwango cha kusema kuwa yuko tayari kwa Olimpiki. Alilalamika kuwa Ogallo alipoteza pigano lake la nusu-fainali kwa sababu refa kutoka Kaskazini mwa Afrika alipendelea Sabah.

Kenya iliwakilishwa na wanaume wanane na wanawake saba kwenye mashindano ya Dakar. Mbali na Ogallo, wanataekwondo wengine kutoka Kenya waliozoa medali ni Mary Muriu na Everlyne Aluoch. Muriu alipata shaba baada ya kulemewa na Mmoroko Lasry Madam kwa alama 15-3 katika nusu-fainali ya uzani wa unyoya. Aluoch alipigwa na Bathily Astana kutoka Ivory Coast 13-6 katika nusu-fainali ya uzani wa kati.

Wapiganaji wengine wa Kenya akiwemo mwanamke wa kwanza kushiriki Olimpiki, Milka Akinyi, hawakupata medali. Akinyi aliwakilisha Kenya kwenye Olimpiki za Beijing nchini Uchina mwaka 2008 akiwa na Dickson Wamwiru ambaye alifariki Septemba 2020.

Marangu alikiri kuwa mashindano ya wanaume mjini Dakar yalikuwa magumu. Aliongeza, “Timu yetu ya wanaume haikufanya vizuri. Nadhani matayarisho yalichangia pakubwa wao kutofanya vyema. Tulianza maandalizi tukiwa tumechelewa…karibu wiki mbili ama tatu kabla ya kuelekea Dakar. Muda haukutosha kujiandaa.”

Kocha huyo alifichua kuwa Ogallo atarejea mazoezini Jumatatu ijayo. Wachezaji wa kufanyisha Ogallo mazoezi kambini Kasarani bado hawajatangazwa.Morocco iliibuka bingwa wa Afrika kwa kuzoa alama 789 baada ya kuvuna medali tatu za dhahabu, fedha sita na shaba nne.

Misri ilikamata nafasi ya pili kwa alama 779 kutokana na dhahabu tatu, fedha tano na shaba sita nayo nambari tatu Ivory Coast inapata alama 681 kwa kuambulia dhahabu tatu, fedha nne na shaba nne. Tunisia ilivuna medali nyingi za dhahabu; nne. Alimaliza mashindano katika nafasi ya nne kwa alama 486 baada pia kupata shaba mbili.

  • Tags

You can share this post!

Mkimbizi Msafiri akimbia kilomita zaidi ya kilomita 500...

Naibu chifu afumaniwa akishiriki ngono na mwanafunzi