Habari MsetoSiasa

Ogiek wataka Rais kuunda jopo kutatua mzozo wa msitu wa Mau

August 25th, 2019 2 min read

NA ERICK MATARA

JAMII ya Ogiek imemwomba Rais Uhuru Kenyatta kuunda jopo ambalo litapendekeza suluhisho la kudumu kuhusiana na utata wa msitu wa Maasai Mau.

Matamshi ya jamii hiyo ndogo ambayo huishi msituni yanajiri huku oparesheni ya kuwatimua wanaoishi ndani ya msitu huo ikinukia baada ya Waziri wa Mazingira, Bw Keriako Tobiko kusema shughuli hiyo itaanza wakati wowote.

Mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Ogiek, Bw Joseph Towett alisema wanaunga mkono oparesheni hiyo inayolenga kutunza msitu huo ambao ni vyanzo vya mito mingi lakini akasema suluhisho la kudumu kuhusu mzozo wa ardhi ya msitu lazima upatikane.

“Ili kumaliza uhasama wa kikabila kati ya jamii mbalimbali zinazoishi karibu na Mau, serikali lazima ibuni jopo kushughulikia mzozo wa ardhi na dhuluma za kihistoria kuhusu nani anaishi ndani au nje ya msitu,” akasema Bw Towett.

Kauli ya wazee hao inajiri siku moja baada ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Bonde la Ufa kuafikiana kuandaa mazungumzo na Bw Tobiko kabla ya oparesheni hiyo haijaanza.

Viongozi hao zaidi 30 wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi kwenye Bunge la Seneti, Bw Kipchumba Murkomen walidai kwamba familia 60, 000 zinazolengwa kwenye oparesheni hiyo zinaishi kwenye ardhi inayosimamiwa na serikali ya Kaunti ya Narok na Shirika la Misitu nchini(KFS) haina haki kutwaa ardhi hiyo.

Wazee wa Ogiek ambao pia waliandaa mkutano mjini Nakuru walishauri serikali kuhamisha familia ambazo zitaathirika katika zaidi ya ranchi tano ambazo hazipo ndani ya msitu wa Mau.

“Suluhu kwa tatizo hili ni kuhamisha familia ambazo zinaishi ndani ya msitu katika ranchi nje ya msitu. Baada ya hayo serikali inafaa kuweka mpaka kisha jamii ziruhusiwe kuishi umbali wa mitaa 100 kutoka mpaka huo kama njia ya kuzima tabia ya watu kuendelea kujitwalia ardhi za msitu,” akaongeza Mzee Towett.

Bw Tobiko wiki jana alishikilia kwamba oparesheni hiyo itaendelea jinsi ilivyopangwa na pia akafutilia mbali vyeti 1,200 vya kumiliki ardhi, akisema vilipatikana kwa njia haramu.

Oparesheni hiyo ambayo ni ya pili tangu mwaka jana italenga maeneo ya Nkoben, Ilmotiok and Ololung’a, Enokishomi,Enoosokon,Nkaroni na Sisian.