Habari za Kitaifa

Ogolla: Azimio yakaba serikali

April 24th, 2024 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya sasa unataka uchunguzi wa kisheria uendeshwe kubaini chanzo cha ajali iliyosababisha kifo cha Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla na wanajeshi wengine tisa mnamo Alhamisi wiki jana.

Kundi la wabunge wa muungano huo pia limependekeza kuwa bunge liteue kamati maalum ya kuchunguza ajali hiyo huku likipinga kamati ya uchunguzi iliyopendekezwa na Rais William Ruto.

Wakiongozwa na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, wabunge wa Azimio walisema hawana imani na kamati ya Rais Ruto.

Wabunge hao wa Azimio pia walielezea wasiwasi wao kuhusu hatua ya Rais Ruto kuteua kamati nyingine mbali na iliyobuniwa na Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen mapema mwezi huu kuchunguza ongezeko la ajali zinazohusisha vyombo vyote vya usafiri angani zikiwemo helikopta za kijeshi.

“Tayari tumeanza kuona dalili za kuzua hofu. Tumegundua Rais Ruto ameteua kundi tofauti la wachunguzi mbali na lile ambalo majina ya wanachama wake yalichapishwa na Waziri Murkomen katika gazeti rasmi la serikali mnamo Aprili 8, 2024,” Bw Wandayi akaongeza.

Alisema hayo Jumanne baada ya mkutano wa Kundi la Wabunge wa Azimio (PG) katika Afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, mtaa wa Upper Hill, Nairobi uliohudhuriwa na vinara wa muungano huo wakiongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

“Mkutano wa Kundi la Wabunge unataka uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo ya helikopta na vifo vya wanajeshi wetu akiwemo Mkuu wa Majeshi Jenerali Ogolla; uchunguzi huo uendeshwe wazi na jopo la wanasheria. Tunapinga uchunguzi unaoendeshwa na wanajeshi pekee huku raia wakifungiwa nje.

“Aidha, tunataka familia za wanajeshi waliokufa ziwakilishwe kwa njia huru katika uchunguzi huo,” Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa Ugunja, akakariri kwenye kikao na wanahabari.

Kiongozi huyo wa Wachache pia alitangaza kuwa Azimio imewateua Mbunge wa Mathare Anthony Oluoch na Seneta wa Kitui Enoch Wambua kuongoza mchakato wa kubuniwa kwa Kamati Maalum ya Pamoja ya Bunge kuchunguza kiini cha ajali hiyo iliyotokea mnamo Aprili 18, 2024.

“Tumeamuru Anthony Oluoch na Seneta Enoch Wambua kuanza mpango wa kutayarisha hoja ya kuunda kamati maalum itakayoshirikisha wawakilishi kutoka Seneti na Bunge la Kitaifa kuchunguza kifo hicho tata cha Jenerali Ogolla na wanejeshi wengine tisa,” Bw Wandayi akaeleza.

Wito wa Azimio unajiri siku moja tu baada ya Rais Ruto kuwahakikishia Wakenya wakati wa mazishi ya Jenerali Ogolla nyumbani kwake Ng’iya, Kaunti ya Siaya, kwamba ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo itatolewa kwa umma.

Dkt Ruto, ambaye pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, alitangaza kuwa uchaguzi huo utaendeshwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

“Nina imani kwamba kundi la KDF likiongozwa na Kapteni Omwenga litaendesha uchunguzi kwa utaalamu wa hali ya juu. Na ningependa kutoa hakikisho hapa leo (Jumapili) kwamba matokeo ya uchunguzi huo wa jeshi yatatolewa kwa umma,” akasema.

Dkt Ruto alisema hayo baada ya viongozi wa eneo la Siaya wakiongozwa na Gavana James Orengo na Seneta Oburu Oginga kuhoji mauaji tata ya watu mashuhuru kutoka eneo la Luo Nyanza.

Baadhi ya watu hao, ambao ripoti za uchunguzi kuhusu vifo vyao hazijatolewa wazi, ni aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Robert Ouko, wakili wa kwanza Mkenya Argwings Kodhek, aliyekuwa Mhadhiri na Mtaalamu wa masuala ya Ugatuzi Odhiambo Mbai, miongoni mwa wengine.

Wakati huo huo, KDF imeahirisha ibada ya ukumbusho wa marehemu Jenerali Ogolla ambayo iliratibiwa kufanywa Ijumaa wiki hii.

Kwenye taarifa ya pamoja na familia ya Ogolla, Waziri wa Ulinzi Aden Duale alisema kuwa tarahe mpya ya hafla hiyo itakayoandaliwa katika Uwanja wa Ulinzi, Lang’ata, itatolewa.

Hata hivyo, Bw Duale mnamo Jumanne hakutoa sababu zilizochangia kuahirishwa kwa ibada hiyo.

Ripoti za Ndubi Moturi, Charles Wasonga na Victor Raballa