Oimeke wa ODM aibuka mshindi wa kiti cha ubunge Bonchari

Oimeke wa ODM aibuka mshindi wa kiti cha ubunge Bonchari

Na RUTH MBULA

MBUNGE mpya wa Bonchari atakuwa Pavel Oimeke wa ODM aliyeibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumanne kwa kuzoa kura  8,049 ikiwa ni asilimia 30 ya kura zilizopigwa.

Afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) eneo la Bonchari Benson Ambuko alimtangaza Bw Oimeke mshindi baada ya usiku wenye shughuli tele za kuhesabu kura.

Aliyeibuka wa pili ni Zebedeo Opore wa Jubilee aliyezoa kura 7,279 (asilimia 27) huku mgombea wa UDA Teresa Bitutu akiwa wa tatu kwa kupata kura 6,964 (asilimia 26). Bi Bitutu ni mjanae wa aliyekuwa mbunge wa Bonchari Oroo Oyioka.

Wagombea wengine 10 walipata kura ambazo zilikuwa ni asilimia tano au chini.

Kwa jumla, ni wapigakura 26,526 (asilimia 50.09) waliojitokeza kupiga kura kati ya idadi jumla ya wapigakura 52,955.

Kura zilizoharibika kwenye vituo vyote 103 zilikuwa 446.

Bw Oimeke, akiwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Gavana wa Kisii James Ongwae, aliwashukuru viongozi kwa kumsaidia kwenye kampeni na kuwashukuru wapigakura kwa kumchagua.

Wagombea wengine kwenye kinyang’anyiro hicho walikwa ni Mary Otara (UGP), Jonah Ondieki (New Democrats), Victor Omanwao (PED), Charles Mogaka (PPK), David Ogega (KSC), Kevin Mosomi wa PDU, na Eric Oigo (National Reconstruction Alliance).

Kiti cha ubunge Bonchari kilisalia wazi baada ya kifo cha mbunge John Oroo Oyioka, mnamo Februari 15, 2021.

You can share this post!

Chipukizi asimulia machafuko ya 2007 yalivyomchochea...

Maafisa wa KDF wahofiwa kuuawa kwa bomu Lamu